August 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UCSAF yapanua wigo huduma za mawasiliano vijijini

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

IMEELEZWA kuwa lengo la Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF),ni kuwaunganisha wananchi wa pembezoni hasa vijijini na huduma bora za mawasiliano ikiwemo simu,intaneti,utangazaji na posta
bila kujali jiografia,hali ya uchumi au kijamii.

Na katika kutimiza lengo hilo ilianza utekekalezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya mawasiliano ya simu na hadi Aprili 2026 makubaliano yalifikiwa kwa kata 2,293 zenye vijiji 5,505 na wakazi zaidi ya milioni 32.7 huku minara 2,324 ilipangwa.

Mkuu wa Kanda ya Ziwa wa UCSAF Fredy Kandonga,akizungumza katika mafunzo ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Mkoa wa Mwanza yaliotolewa na mfuko huo na yaliofanyika wilayani Ilemela mkoani humo

Akizungumza Agosti 10,2026 katika mafunzo ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Mkoa wa Mwanza yaliotolewa na mfuko huo na yaliofanyika wilayani Ilemela mkoani humo,Mkuu wa Kanda ya Ziwa wa UCSAF Fredy Kandonga amesema,huduma imekamilika katika kata 2,012 zenye vijiji 5,132,wakazi takribani milioni 29.7,wanapata huduma kupitia minara 2,158.

Kandonga amesema,kwa Kanda ya Ziwa, takribani minara 414 imejengwa katika kata zipatazo 380 za Mikoa ya Mwanza,Simiyu,Mara,Shinyanga,Geita na Kagera.

Ambapo amesema,awamu ya 10 ya mradi wa mawasiliano utekelezaji wake unaendelea katika kata 287 zenye vijiji 359,huku minara 287 inajengwa na wakazi takribani milioni 2.9 wanatarajiwa kunufaika.

“Ruzuku ya Serikali ni takribani sh.bilioni 29,mradi unatarajiwa kukamilika Machi 2027.Hadi sasa minara 7 imewashwa na wananchi wanapata huduma kupitia minara hiyo.Kanda ya Ziwa minara 67 inajengwa huku mnara 1 tayari umewashwa,”amesema Kandonga.

Pia amesema,katika awamu hiyo ya 10 ya mradi wa mawasiliano kwa Kanda ya Ziwa Mkoa wa Geita inajengwa minara 7,Kagera minara 14,Mara minara 11,Mwanza minara 21,Shinyanga minara 6 na Simiyu minara 8.

Sanjari na hayo Kandonga amesema,mradi wa kuboresha uwezo wa minara kutoka kasi ya 2G kwenda kasi ya 2G/3G/4G umetekelezwa kwa lengo la kuongeza uwezo wa wananchi kupata intaneti yenye ubora zaidi.

Amesema,mradi huo unawezesha matumizi ya elimu mtandao,afya mtandao,biashara mtandao na huduma za kifedha kupitia simu ambapo minara 431 imeboreshwa kutoka 2G kwenda 2G/3G/4G huku ruzuku ya Serikali ni sh.bilioni 9.14.

Hata hivyo amesema,miradi hiyo inaonesha mabadiliko katika upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini, hasa katika maeneo ambayo wananchi walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya mtandao wa simu na huduma za intaneti.

Huku uwepo wa mawasiliano ukiongeza fursa za wananchi kutumia simu na intaneti katika biashara,huduma za fedha,mawasiliano ya dharura,elimu na kupata taarifa za masoko.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo yaliotolewa na UCSAF kwa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Mkoa wa Mwanza

Vilevile Kandonga amesema,uwekezaji huo unaenda sambamba na jitihada za kupanua matumizi ya teknolojia katika huduma za Serikali na sekta binafsi,hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.

“UCSAF itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya umma na binafsi kufikia Tanzania ya kidijitali.Tupo tayari kushirikiana na wadau wote wakiwemo Wahariri wa Habari,kubaini na kutatua changamoto za mawasiliano nchini,”amesisitiza Kandonga.