Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
TAASISI ya Mwanangu Development Tanzania (MWADETA) imetoa wito kwa Serikali kuongeza idadi ya walimu wa elimu maalumu ili kuwepo uwiano unaofaa kati ya walimu na wanafunzi wenye mahitaji maalumu, hatua itakayosaidia kuboresha utoaji wa elimu na huduma kwa watoto hao.
Wito huo umetolewa Agosti 7,2026 Wito na Mkurugenzi wa MWADETA, Walter Miya, wakati taasisi hiyo ilipoanza programu ya kuwajengea uwezo walimu wa vitengo maalumu pamoja na Maofisa Elimu Kata wa shule za awali na msingi wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.
Ambapo amesema,uwiano wa walimu na wanafunzi bado si mzuri na kwamba Serikali inapaswa kuongeza wigo wa walimu wa vitengo maalumu kwani shule jumuishi zinahitaji kuzingatia mahitaji maalumu, ikiwemo kuwa na madarasa yenye idadi ndogo ya wanafunzi, vyoo vilivyo karibu na madarasa na walimu wanaoweza kutoa huduma ya karibu kwa wanafunzi.
Ameongeza kuwa,katika kupanga shule jumuishi, halmashauri zinapaswa kuchagua shule zinazoweza kuwekewa mazingira hayo badala ya kutarajia shule zote kuwa jumuishi kwa wakati mmoja.
Sanjari na hayo,amesema,mafunzo hayo yamelenga kuwapa elimu walimu na Maofisa Elimu Kata kuhusu namna ya kuwatambua watoto wenye changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi wanapoletwa shuleni, pamoja na namna ya kuwahudumia katika mazingira ya shule.
Pia amesema,changamoto kubwa walioibaini ni idadi ndogo ya watoto wenye hali hiyo wanaohudhuria shule huku watoto wengine hubaki nyumbani kutokana na kukosa huduma muhimu, ikiwemo msaada wa kujisaidia haja, hali inayoweza kuwafanya waone aibu na kuacha kwenda shule licha ya kuwa na uwezo wa kujifunza.
Ofisa Elimu Maalumu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Sarah Ulimboka amesema, halmshauri hiyo ina walimu 55 wa elimu maalumu na mahitaji ni walimu 105 huku ikiwa na wanafunzi wenye mahitaji maalumu mbalimbali 1050,hali inayodhihirisha umuhimu wa kuongeza walimu kulingana na idadi na aina za mahitaji ya wanafunzi.
Ulimboka amesema,Serikali imeendelea kuajiri walimu waliobobea katika elimu maalumu ambapo kwa mwaka huu halmshauri hiyo imepokea walimu saba ambao tayari wamepangiwa katika shule zenye mahitaji hayo.
“Sera ya elimu inaelekeza uwiano wa walimu na wanafunzi kulingana na aina ya ulemavu, mfano kuwa mwalimu anayefundisha wanafunzi wenye uziwi anafaa kuwa na wanafunzi watano, mwenye ulemavu wa akili wanafunzi watano na mwanafunzi mwenye usonji mwalimu mmoja.
Kwa upande wake Ofisa Elimu Kata ya Pamba Edina Kajungu amesema,kupitia mafunzo hayo atatoa elimu kwa viongozi wa Serikali za Mitaa na jamii ili watoto wenye mahitaji maalumu wanaozaliwa na kubaki nyumbani watambuliwe, badala ya kufichwa pamoja na kupelekwa shuleni au hospitalini kupata huduma za afya na elimu.
Amesema pia kuna umuhimu wa walimu kufundishwa zaidi mbinu za kuwahudumia watoto wenye changamoto ya mgongo wazi, ikiwemo matumizi ya vifaa vinavyowasaidia wanapokuwa shuleni pamoja na namna za kuwasaidia kutoa haja.
Naye Salama Yusuph mama wa mtoto mwenye chamangamoto ya mgongo wazi amesema,wazazi wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa na walimu wenye ujuzi katika baadhi ya shule za Serikali, hali inayowalazimu kuwapeleka watoto wao katika shule binafsi kwa gharama kubwa.
Ameiomba Serikali kuongeza walimu wa elimu maalumu katika shule za Serikali ili watoto wenye mahitaji maalumu wapate elimu na huduma muhimu, ikiwemo kusaidiwa kujisaidia haja, kwani kukosa huduma hiyo kunaweza kuwaweka katika hatari ya kupata magonjwa.

More Stories
Rushwa yatakiwa kukomeshwa kabla watoto hawajajifunza kuipenda
Prof.Kabudi ahimiza matumizi teknolojia za kisasa katika uzalishaji
Chongolo aitaka NIRC kukamilisha ugawaji wa Pampu za Umwagiliaji