August 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mamlaka ya maji Mbeya yaonya wanaoiba mifuniko

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Mbeya

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mbeya (MBEYA UWSA) imeonya baadhi ya watu wanaojihusisha na wizi wa mifuniko ya chemba za maji taka na kuiuza kama vyuma chakavu, ikisema tabia hiyo inaweza kuhatarisha usalama wa wananchi na kuchafua mazingira.

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Neema Stanton, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Mbeya.

Stanton amesema wizi wa mifuniko ya chemba za maji taka umeendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo, hali inayosababisha chemba hizo kuwa wazi na hivyo kuongeza hatari kwa wananchi pamoja na kuchangia uchafuzi wa mazingira.

“Unapofunua chemba tayari unasababisha uchafu kwenye jiji letu ambalo tunahitaji liwe safi. Pia, watu wengine wanapoona chemba zikiwa wazi hutumia nafasi hiyo kutupa taka,” amesema Stanton.

Amesema wananchi wanapaswa kutoa taarifa kwa mamlaka mara wanapobaini chemba zimeachwa wazi, zimeziba au mifuniko yake imeibiwa ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.

Stanton ametoa wito kwa wananchi wa Jiji la Mbeya na Mji wa Mbalizi kushirikiana na mamlaka katika kulinda miundombinu ya maji taka na kuhakikisha mazingira yanabaki safi.

Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa kuhusu watu wanaoharibu au kuiba mifuniko ya chemba, akieleza kuwa wizi huo umeendelea kuwa changamoto katika baadhi ya maeneo.

“Tunawaomba wananchi tushirikiane na kuwafichua watu wanaoiba mifuniko ya chemba. Pia tunaomba wafanyabiashara wa vyuma chakavu wasinunue mifuniko hiyo kwa sababu kufanya hivyo kunachochea wizi wa miundombinu ya maji taka,” amesema.

Amesema ushirikiano kati ya wananchi, mamlaka na wafanyabiashara wa vyuma chakavu ni muhimu katika kukomesha vitendo vya uharibifu na kuhakikisha miundombinu ya maji taka inalindwa kwa manufaa ya jamii.