Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online-Mbeya
HALMASHAURI ya Wilaya ya Busokelo mkoani Mbeya imejipanga kuendelea kutoa elimu ya lishe kwa jamii, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na tatizo la udumavu kwa watoto.
Imeelezwa kuwa licha ya upatikanaji wa chakula kuwa mzuri katika maeneo mengi ya wilaya hiyo, suala la udumavu bado limeendelea kuwa changamoto kutokana na baadhi ya wazazi kujikita zaidi katika shughuli za utafutaji wa kipato na kushindwa kuzingatia ipasavyo lishe ya watoto.

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo, Mwanahawa Musa,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya lishe katika halmashauri hiyo kuelekea kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane inayofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Mwanahawa amesema,Maofisa Lishe kutoka Idara ya Afya wamekuwa wakitoa elimu kwa wazazi, hususani akina mama, kuhusu umuhimu wa lishe bora na namna ya kuhakikisha watoto wanapata chakula chenye virutubisho muhimu.
Amesema,wamekuwa wakishirikisha viongozi wa dini na wahudumu wa afya katika kutoa elimu hiyo kwa jamii, ikiwemo kuhamasisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa watoto katika miezi sita ya kwanza.
Pia amesema,baadhi ya wananchi wa Busokelo wamekuwa wakipata changamoto katika kuzingatia ushauri huo kutokana na imani kwamba mtoto anapofikisha umri wa miezi mitatu anahitaji kuanza kupewa vyakula vingine.
Hata hivyo amesema,maziwa ya mama yanatosheleza mahitaji ya mtoto katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo na yana virutubisho muhimu kwa ukuaji na maendeleo yake.
Aisha amesema,halmashauri hiyo itaendelea kutoa elimu ya lishe katika jamii, ikiwemo kupitia nyumba za ibada, ili kuongeza uelewa wa wazazi na walezi kuhusu lishe bora ya watoto.
Hata hivyo amesema, halmshauri hiyo ina upatikanaji mzuri wa vyakula mbalimbali, lakini changamoto kubwa ipo katika namna ya kupanga mlo unaokidhi mahitaji ya lishe ya mtoto.
Kwa upande wake, Rose Adam, mkazi wa Kata ya Ilomba jijini Mbeya amesema,baadhi ya wazazi bado hawajazingatia kikamilifu suala la lishe ya watoto kutokana na kutumia muda mwingi katika shughuli za kutafuta kipato.
“Mimi nimekuja kwenye maonesho haya kupata elimu.Suala la lishe kwa wazazi wengi bado hatulizingatii ipasavyo kwa sababu muda mwingi tupo kwenye utafutaji. Hili halipingiki kabisa, tubadilike ndugu zangu wazazi na walezi kwa sababu watoto wanadumaa sana,” amesema.


More Stories
COPRA yazindua jarida kuongeza uelewa wa fursa kilimo
Mamlaka ya maji Mbeya yaonya wanaoiba mifuniko
EWURA yaonya wanaofanya biashara bila leseni