August 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WRRB Yapongezwa kwa Maandalizi ya Mnada wa Mifugo




MKURUGENZI wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Needpeace Wambuya, ameipongeza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kwa kasi ya utekelezaji wa majukumu yake, hususan hatua ya kuanzisha mpango wa kuuza mifugo kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.


Wambuya ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la WRRB katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea kwenye Viwanja vya John Malecela jijini Dodoma leo, Agosti 2, 2026.


“Niwapongeze sana kwa kazi nzuri mnayofanya. Nimeona mpango wenu wa kuingiza mifugo kwenye Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, na ninaamini mnafikia hatua nzuri za utekelezaji,” amesema Wambuya.


Kwa upande wake, Ofisa Leseni wa WRRB, Nasri Khea, amesema maandalizi ya mnada wa kwanza wa mifugo kupitia mfumo huo yamekamilika kwa kiasi kikubwa, huku mnada huo ukitarajiwa kufanyika hivi karibuni katika Wilaya ya Mvomero.


Khea ameongeza kuwa WRRB inaendelea kupanua matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa kuingiza bidhaa mbalimbali, zikiwemo mwani na mahindi, ili kuongeza fursa za biashara na masoko kwa wazalishaji.