August 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tusumuke Group yaonyesha teknolojia bora za kuku

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online

WAFUGAJI na wadau wa sekta ya mifugo wamehimizwa kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa vya ufugaji wa kuku ili kuongeza tija, kudhibiti magonjwa na kuboresha usafirishaji wa kuku, huku wakikaribishwa kutembelea banda la Tusumuke Group lililopo katika banda kubwa la   Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Akizungumza katika maonesho ya wakulima na wafugaji (Nanenane ) , mwakilishi wa Tusumuke Group, Christopher Dionies, alisema kampuni hiyo imeleta vifaa mbalimbali vinavyorahisisha ufugaji wa kuku, ikiwemo mifumo ya maji, mabanda ya kisasa ya cage system yanayotumia nafasi ndogo lakini kuhifadhi idadi kubwa ya kuku, pamoja na mashine ya FOGO inayotumika kupunguza joto bandani na kufanya usafi wa mabanda kwa njia ya kufukiza dawa ili kuzuia milipuko ya magonjwa.

Alisema hatua hiyo inakuja sambamba na uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Taifa wa Ufugaji wa Kuku wa Miaka Kumi uliozinduliwa na Waziri Mkuu wakati wa maadhimisho ya Nanenane, ukilenga kuongeza tija na maendeleo katika sekta ya ufugaji wa kuku nchini.

Magesa alieleza kuwa banda hilo pia linatoa elimu kuhusu matumizi ya mashine za kutotolesha vifaranga zinazotumia umeme, betri na nishati ya jua, kuanzia uwezo wa kutotolesha mayai 30 na kuendelea, ili kuwasaidia wafugaji kupata vifaranga bora na kuongeza kiwango cha mafanikio katika utotoleshaji.

Aidha, alisema wameleta vyakula vya kuku pamoja na vibebeo maalumu vya plastiki kwa ajili ya usafirishaji wa kuku, akibainisha kuwa matumizi ya matenga na vifungashio visivyo salama yamekuwa yakisababisha majeraha na vifo vya kuku baada ya kusafirishwa.

Aliwataka wafugaji na wananchi kutembelea banda la Wizara ya Mifugo pamoja na banda la Tusumuke Group wakati wa Maonesho ya Nanenane ili kujifunza teknolojia mbalimbali za kisasa zinazoweza kuongeza uzalishaji na kuboresha biashara ya ufugaji wa kuku nchini.