August 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwigulu:TADB ni muhimu kuongeza uzalishaji wa kilimo

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WAZIRI Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ameielekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuongeza uwezo wake wa kifedha na kupanua wigo wa utoaji wa mikopo ili kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi nchini, akisema hatua hiyo itachochea mageuzi ya sekta ya kilimo na kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la TADB katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Dodoma, leo Agosti Mosi ,2026 Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaiona TADB kuwa chombo muhimu cha kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wazalishaji na wawekezaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi. Alisisitiza kuwa kuimarishwa kwa benki hiyo kutaiwezesha kujibu mahitaji yanayoongezeka ya wadau wa sekta hizo.

Amesema Serikali haiwezi kutegemea ruzuku pekee kila mwaka katika kuendeleza sekta ya kilimo, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na taasisi imara ya kifedha inayowezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kupata mikopo kwa wakati ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.

Waziri Mkuu pia aliitaka TADB kuongeza uwezo wa kufadhili ununuzi wa mbolea, pembejeo, zana za kisasa za kilimo na miradi ya kuongeza thamani ya mazao, akieleza kuwa uwekezaji huo utaongeza tija, ushindani wa bidhaa za Tanzania na kipato cha wazalishaji.

Aidha, alielekeza benki hiyo kushirikiana kwa karibu na Wizara za Kilimo na Mifugo pamoja na TAMISEMI kuwekeza katika miundombinu ya baada ya mavuno, hususan ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao. Alisema hatua hiyo itaimarisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kuwawezesha wakulima kupata mikopo kwa kutumia mazao yao kama dhamana.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege,amesema benki hiyo imeendelea kutekeleza jukumu lake la kufadhili miradi ya kimkakati inayochochea maendeleo ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, huku zaidi ya shilingi bilioni 700 zikiwa zimetolewa kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji nchini.

Amesema mazao ya kahawa kutoka mikoa ya Kagera na Kigoma kupitia vyama vya ushirika ni miongoni mwa mafanikio yaliyowavutia wadau wengi waliotembelea banda la TADB katika maonesho hayo, jambo linaloonesha mchango wa benki hiyo katika kuongeza thamani ya mazao na kuwawezesha wakulima.

Nyabundege aliongeza kuwa TADB imewezesha pia mradi wa kisasa wa ufugaji na uchakataji wa samaki uliopo Bagamoyo unaotumia teknolojia kutoka Misri wenye uwezo wa kuhifadhi hadi tani 90 za samaki kwa mwezi. Alisema uwekezaji huo umechangia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, kuokoa fedha za kigeni, kuongeza ajira kwa Watanzania na kuimarisha mchango wa sekta ya kilimo na uvuvi katika ukuaji wa uchumi wa taifa.