July 31, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chatanda sasa mlezi wa CCM Mara

NA: MWANDISHI WETU

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu (MCC), Mary Chatanda, amebadilishwa mkoa wa ulezi wa kichama na sasa ni mlezi wa CCM mkoa wa Mara.

Mabadiliko hayo yamefanyika Julai 29, 2026, Zanzibar, kufuatia vikao vya Chama vinavyoendelea. Kabla ya mabadiliko hayo, Chatanda alikuwa mlezi wa mikoa ya Mjini na Magharibi, Zanzibar.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Chatanda amekishukuru Chama chake kwa kuendelea kumuamini kutekeleza majukumu mbalimbali ya kichama.

“Nimepokea taarifa hii ya mabadiliko ya ulezi wa Chama mkoa kwa moyo wa unyeyekevu. Nakishukuru Chama changu kwa kuniamini. Niwaombe wanachama wenzangu na wananchi kwa ujumla tushirikiane kuhakikisha tunasukuma mbele gurudumu la maendeleo na Chama chetu”.

Ameongeza kuwa “Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imepeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo mkoani Mara, ni wajibu wetu kuhakikisha fedha hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa katika kuboresha maisha ya wananchi”.

Akiwa mlezi mkoani humo, pamoja na mambo mengine, Chatanda anawajibika kuwaunganisha wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla.

Aidha, kuimarisha uhai wa Chama, kuongeza idadi ya wanachama na kuhimiza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Vilevile, anawajibika kujenga uhusiano mzuri baina ya Chama na serikali.

Mkoa wa Mara unaundwa na wilaya sita ambazo ni Bunda, Butiama, Musoma, Rorya, Serengeti na Tarime