July 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani waagiza ziara ya dharura mgodini kisa mapato

Na Moses Ng’wat, Mbozi.

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi limeagiza kufanyika kwa ziara ya dharura katika Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Magamba, Wilayani humo, baada ya kuibuka hofu kuhusu mwenendo wa ukusanyaji wa mapato yanayotokana na shughuli za mgodi huo.

Uamuzi huo ulifikiwa Julai 28, 2026, katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri , wakati wa kupokea na kujadili taarifa za Kata kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Katika kikao hicho, madiwani walihoji uhalisia wa takwimu za uzalishaji wa makaa ya mawe ukilinganisha na kiwango cha mapato kinachoingizwa katika Halmashauri, wakitaka kufanyika kwa ukaguzi wa kina kubaini changamoto zinazoweza kusababisha upotevu wa mapato ya umma.

Mjadala huo uliibuliwa na Diwani wa Kata ya Magamba, Charles Mbagwa, na Diwani wa Kata ya Bara, Aloyce Mdalavuma, waliotaka ufafanuzi kuhusu kiasi halisi cha makaa ya mawe kinachozalishwa, kusafirishwa pamoja na mapato yanayokusanywa kutokana na shughuli za mgodi huo.

Baada ya mjadala huo, Baraza hilo liliamua kuikabidhi Kamati ya Fedha, Mipango na Uchumi kufanya ziara hiyo ili kujiridhisha na hali halisi ya uzalishaji na mapato yanayowasilishwa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Maarifa Mwashitete, alisema Halmashauri haitasita kuchukua hatua za kisheria na kiutendaji dhidi ya mtendaji au afisa yeyote atakayebainika kushirikiana na wawekezaji katika kuhujumu mapato ya serikali.

Alisema usimamizi madhubuti wa rasilimali zilizopo ndani ya wilaya hiyo ni muhimu katika kuongeza mapato ya ndani na kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zinazozalishwa katika maeneo yao

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbozi, Majaliwa Mlawizi, aliwataka madiwani kuwa na msimamo mkali katika kulinda rasilimali za taifa, hususan zinazohusiana na madini na kuhakikisha zinatumika kwa manufaa ya wananchi.

Aliwataka madiwani kufika katika maeneo yote wanayoona kuna shughuli za uchimbaji wa rasilimali hizo ili kujiridhisha na mwenendo wa shughuli hizo na kuhakikisha serikali inapata mapato yanayostahili.

Mlawizi alisema haiwezekani katika wilaya yenye viongozi wa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama, mwekezaji akaingia na kuanza kufanya shughuli bila mamlaka husika kufahamu kinachoendelea.

Akitoa salamu za serikali katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, aliwapongeza madiwani kwa ushirikiano wao katika kusimamia maendeleo na ukusanyaji wa mapato katika wilaya hiyo.

Mbega alisema ushirikiano kati ya madiwani na wataalamu wa halmashauri umeiwezesha Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kufikia asilimia 140 ya lengo la ukusanyaji wa mapato katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Alisisitiza kuwa ukusanyaji wa mapato uendelee kufanyika kwa kuzingatia utu na ubinadamu, bila kuwaumiza wananchi na walipa kodi wanaochangia maendeleo ya halmashauri.

Kwa upande mwingine, Mbunge wa Jimbo la Vwawa, Japhet Hasunga, pamoja na viongozi wengine, walisisitiza umuhimu wa shughuli zote za kiuchumi kufanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kulinda maslahi ya wananchi na mazingira.