Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya
WAKULIMA wengi katika Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya, wanaendelea kuelekeza nguvu zao kwenye kilimo cha alizeti kutokana na gharama zake ndogo za uzalishaji na faida kubwa zinazopatikana baada ya mavuno, tofauti na baadhi ya mazao ya biashara yanayohitaji mtaji mkubwa.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Athuman Bamba amesema alizeti imeendelea kuwa zao linalovutia wakulima wengi kwa sababu halihitaji gharama kubwa za uzalishaji wala matunzo mengi ikilinganishwa na zao la tumbaku.
Amesema wakati tumbaku hulimwa katika kata tisa pekee za wilaya hiyo, alizeti hulimwa katika kata zote 20 kutokana na urahisi wake wa uzalishaji na manufaa yake kwa wakulima.
“Alizeti imekuwa na tija kubwa kwa wakulima kwa sababu haina mlolongo mrefu wa matunzo. Baada ya kupanda, mkulima hufanya matunzo machache hadi zao linapokomaa, tofauti na mazao mengine yanayohitaji gharama na uangalizi mkubwa,” amesema Bamba.
Amesema wakulima wengi wameendelea kulikumbatia zao hilo kwa kuwa huwapatia mafuta ya matumizi ya nyumbani, huku ziada ya mavuno ikiuzwa na kuwa chanzo cha kipato cha kugharamia mahitaji ya familia, ikiwemo ada za watoto.
Kwa mujibu wa Bamba, alizeti ni moja ya mazao ya biashara yanayochangia mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, ambapo halmashauri hukusanya ushuru wa asilimia tatu kwa kila gunia la alizeti, sawa na utaratibu unaotumika kwa zao la tumbaku, ingawa kiwango cha uzalishaji na mapato hutofautiana.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuunga mkono uzalishaji wa zao hilo kwa kuwapatia baadhi ya wakulima mbegu bora katika mwaka 2025 ili kuongeza uzalishaji na tija.
Bamba amesema alizeti ni zao la kimkakati kwa Wilaya ya Chunya na limeendelea kuwa miongoni mwa mazao yanayochangia kwa kiwango kikubwa mapato ya halmashauri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya,Gideon Mapunda amesema uchumi wa wilaya hiyo unategemea kwa kiasi kikubwa sekta ya kilimo na mifugo.
Amesema mazao makuu ya chakula ni mahindi, huku mazao ya biashara yakiwa alizeti na tumbaku, akibainisha kuwa pamoja na kukua kwa uzalishaji wa alizeti, tumbaku bado inaendelea kuwa zao muhimu katika uchumi wa wilaya.
Naye mkulima wa alizeti kutoka Kata ya Lupa, Estlia Juma amesema kilimo hicho kimebadilisha maisha yake kutokana na gharama zake ndogo na urahisi wa kukiendesha.
“Nashukuru sana kilimo cha alizeti kwa sababu hakihitaji gharama kubwa. Mara nyingi hakitumii mbolea nyingi, na baada ya kupanda matunzo yake ni machache. Hii ndiyo sababu wakulima wengi wanakimbilia kulima alizeti,” amesema Estlia.

More Stories
HGWT yaahidi kutekeleza mkakati wa kutokomeza ukeketaji
Askari wanyamapori Babati wapata mafunzo
Mafunzo ya kuongelea kiwango cha kimataifa kutolewa bure Dar