July 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakala wa Vipimo washiriki NBC Marathon Dodoma

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Watumishi wa Wakala wa Vipimo (WMA) asubuhi ya leo Julai 26, 2026 wameshiriki katika mbio za NBC Marathon zilizozofanyika jijini Dodoma kwa uratibu wa Benki ya NBC.

Lengo kuu la mbio hizo ilikuwa kukusanya fedha za kusaidia matibabu kwa wagonjwa wasiojiweza, pamoja na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa mazoezi katika kuimarisha afya.

WMA imeshiriki katika mbio hizo kuunga mkono dhamira hiyo ya kibinadamu na kuonyesha mchango wa taasisi za Serikali katika masuala ya afya na ustawi wa jamii.

Katika ushiriki huo, watumishi 6 wa WMA walikimbia umbali wa Kilometa 10 wakati mtumishi 1 alikimbia Kilometa 21.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba amewapongeza washiriki na waandaaji wa mbio hizo.

Aidha ametoa wito kwa Watanzania kushiriki kwa wingi katika matukio kama haya ili kufanikisha malengo ya kuwasaidia wagonjwa na kuimarisha afya ya Taifa.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa WMA, Meneja wa Mkoa wa Dodoma, Ibrahim Saidi amesema, “Tumeshiriki ili kusapoti lengo la NBC Marathon la kusaidia wenzetu wanaohitaji matibabu.

Pia tunahamasisha Watanzania kudumisha afya kupitia mazoezi ili tuweze kutoa huduma bora kwa umma.”