Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline.Dodoma
JESHIi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma limethibitisha kuwa limejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wa washiriki zaidi ya 13,000 watakaoshiriki NBC Dodoma Marathon itakayofanyika Julai 26, 2026 katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma, SSP Yusufu Kamota, amewataka madereva wa magari yanayopita Dodoma kutumia Dodoma Ring Road ili kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji na kuruhusu mbio kufanyika kwa usalama.
Aidha, wananchi ambao hawana ulazima wa kutumia magari yao siku hiyo wametakiwa kuyaacha nyumbani ili kusaidia kupunguza foleni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa NBC, Godwin Semunyu, amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha washiriki wanapata huduma bora kabla, wakati na baada ya mbio.

Miongoni mwa huduma hizo ni TRC kuongeza safari maalum ya treni saa 1:00 jioni kutoka Dodoma kuelekea Morogoro na Dar es Salaam, Vodacom Tanzania kutoa huduma ya Wi-Fi na kuimarisha mtandao wa mawasiliano, huku GSM Group ikitoa maji na juisi kwa washiriki.
Mhe. Waziri Mkuu Mwigulu Lameck Nchemba (Mb.) anatarajiwa kuongoza washiriki wa mbio hizi zinazolenga kukusanya Shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kupunguza vifo vya akina mama na watoto wakati wa kujifungua, kusaidia upasuaji wa watoto wenye matatizo ya moyo, na kuimarisha huduma za upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu.


More Stories
Kampuni ya Oryx Gas yakabidhi mitumgi 600 kwa wajasiriamali
DCEA yafanikiwa kuteketeza ekari 291.2 Mara
Manyire waanza ujenzi Sekondari mpya