
Na Moses Ng’wat, Mbozi.
WATENGENEZA maudhui 25 (influencers) Mkoani Songwe wamehitimisha mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) kupitia mradi wake wa Dumisha Amani Awamu ya Pili, unaotekelezwa kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo washiriki kutumia majukwaa ya kidijiti kueneza ujumbe wa amani, kuimarisha mshikamano wa jamii na kujiongezea kipato kupitia utengenezaji wa maudhui yenye tija.
Akizungumza wakati wa kufungwa kwa mafunzo hayo, Ofisa wa Mradi wa Dumisha Amani, kutoka UNDP, Edmund Mbigili, alisema watengeneza maudhui hao walichaguliwa kutokana na ushawishi mkubwa walionao katika jamii kupitia mitandao ya kijamii, jambo linalowapa nafasi ya kuelimisha wananchi na kuhamasisha amani.

Mbigili alisema mradi huo unafadhiliwa na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kujenga Amani (UN Peacebuilding Fund) kupitia Mfuko Mdogo wa Amani na Usalama wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Alisema mafunzo hayo yamewapa washiriki ujuzi wa kutumia mitandao ya kijamii kwa njia chanya ili kuhamasisha amani, usalama na mshikamano wa kitaifa, sambamba na kuitumia kama fursa ya kujiongezea kipato kwa kuzalisha maudhui yenye manufaa kwa jamii.

Aliongeza kuwa baada ya mafunzo hayo, washiriki wanatarajiwa kuendesha kampeni za kidijitali zitakazohamasisha wananchi kulinda amani, usalama na utulivu wa nchi, hususan katika maeneo ya mipakani.
“Tunataka vijana hawa watumie ushawishi wao kueneza ujumbe wa amani na mshikamano badala ya maudhui yanayoweza kupotosha jamii, pia mitandao ya kijamii inaweza kuwa chombo muhimu cha kujenga taifa lenye utulivu endapo itatumika kwa uwajibikaji,” alisema Mbigili.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walisema elimu waliyoipata itawasaidia kuboresha maudhui wanayozalisha na kuyafanya yawe na mchango chanya katika jamii.

Mmoja wa washiriki, Getruda Halinga, alisema mafunzo hayo yatamwezesha kutumia majukwaa yake ya kidijitali kuhamasisha amani huku akiongeza idadi ya wasomaji na wafuasi wake.
Naye, Japhet Hayola, alisema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwa kuwa yatawawezesha watengeneza maudhui kuandaa kazi zenye tija zinazozingatia sheria, maadili na miongozo ya matumizi ya mitandao ya kijamii.
Mafunzo hayo ni sehemu ya kampeni ya muda mrefu ya UNDP nchini Tanzania inayolenga kuimarisha amani katika mikoa ya mipakani. Katika awamu ya pili ya mradi wa Dumisha Amani, mafunzo hayo yamefanyika katika mikoa ya Songwe, Mbeya, Mwanza na Geita.


More Stories
Matukio katika picha wahitimu Chuo cha Ulinzi
Waziri Ndejembi azindua mradi wa njia ya kusafirisha Umeme, Masasi hadi Newala
Serikali yatangaza neema kwa wakulima