November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maeneo yatayofutiwa hati kutumika kwa michezo

Na Omary Mngindo, TimesMajira Online, Bagamoyo

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Muharami Mkenge, ameahidi kufuatilia maeneo yasiyoendelezwa ili yafutiwe hati zake na baadhi yao yaelekezwe katika ujenzi wa viwanja vya michezo.

Mkenge ameyasema hayo katika Kata ya Mapinga kwenye mkutano wake wa Kampeni baada ya wananchi kutoa kilio chao cha muda mrefu cha uwepo wa mapori yasiyoendelezwa, huku wakazi wakikosa maeneo kwa ajili ya shughuli za kijamii sanjali na kukosa viwanja vya michezo.

Mara baada ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa Kata hiyo amesema, licha ya kukosekana kwa maeneo kwa ajili ya shughuli muhimu za kijamii ikiwemo shule, zahanati na huduma nyingine ikiwemo viwanja kwa ajili ya sekta ya michezo lakinikuna maeneo
ambayo bado ni mapori, hivyo nitayashughulikia na kuomba vibali ili yatumike kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Amesema kuwa, katika maeneo mengi vijana wanakabiliwa na changamoto ya viwanja vya michezo hivyo atakapochaguliwa kuwa mbunge pamoja na shughuli mbalimbili za kimaendeleo pia atahakikisha maeneo yasiyoendelezaa atayafikisha kwa Rais yafutiwe hati ili mengine yatumike kwa viwanja vya michezo.

“Niwaombe Wanamapinga ikifika Oktoba 28 tujitokeze kwa wingi kuwachagua wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuanzia nafasi ya Urais Dkt. John Magufuli, mimi Mkenge Ubunge na Chandika Udiwani ili kwa pamoja tukafanye kazi ambayo tayari imeshaanzishwa na waliotangulia,” alisema Mkenge.

Pia amesema kuwa, moja ya azma yake ni kuwepo kwa Ligi ya Mbunge jimbo la Bagamoyo, na pasipokuwepo na viwanja vya kutosha kunaweza kukwamisha juhudi mipango hiyo na kuwafanya vijana kushindwa kufikia ndoto zao katika soka.

“Mtangulizi wangu Dkt. Shukuru Kawambwa katika vipindi vyake vya Ubunge alijitoa kwa kiasi kikubwa katika ligi ya Mbunge iliyojulikana kwa jina la Kawambwa Cup, nami nitafuata nyayo hizo, vijana mtuunge mkono kwani pia nitawahamasisha madiwani yaanzie ngaza za Kata nasi tutahakikisha tunafuatili na kupata maeneo ambayo yatatumika kwa ajili ya ujenzi wa viwanja,” amesema Mkenge.