November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mchungaji James Chimbalambala (wa pili kulia) akitoa historia ya kiwanja chake kwa wataalam wa sekta ya ardhi katika mtaa wa Mji Mpya eneo la Kanisani Halmashauri ya Mji wa Babati, wakati wa utekezaji zoezi la elimu ya kodi ya pango la ardhi nyumba kwa nyumba mwishoni mwa wiki. .

Wizara ya Ardhi yabisha hodi nyumba kwa nyumba nchini

Na Eliafile Solla, TimesMajira Online

SIKU ya elimu ya mlipa kodi ya pango la ardhi imetajwa kuwa mwarobaini katika utatuzi wa migogoro ya ardhi hasa migogoro inayohusiana na mipaka ya viwanja pamoja na ile ya upimaji.

Mchungaji James Chimbalambala (wa pili kulia) akitoa historia ya kiwanja chake kwa wataalam wa sekta ya ardhi katika mtaa wa Mji Mpya eneo la Kanisani Halmashauri ya Mji wa Babati, wakati wa utekezaji zoezi la elimu ya kodi ya pango la ardhi nyumba kwa nyumba mwishoni mwa wiki.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Manyara,Leonardd Msafiri alipokutana na kikosi kazi maalum kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kutoa elimu ya kodi ya pango la ardhi pamoja na masuala mengine yahusuyo sekta ya ardhi katika Mkoa wa Manyara.

Akizungumza katika utekelezaji wa zoezi hilo la utoaji elimu ya kodi nyumba kwa nyumba, Msafiri alisema wizara iligatua madaraka kwa maana ya kusogeza huduma karibu na mteja kutoka kuwa na ofisi za ardhi za kanda ambazo zilikuwa nane nchi nzima na kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa kwenye kila mkoa katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Msafiri amesisitiza kwamba, wizara imepiga hatua kubwa kuanzisha kampeni ya siku ya elimu ya mlipa kodi kwa sababu utoaji elimu nyumba kwa nyumba unawapa fursa ya kukutana na wateja wao moja kwa moja na pia wanagundua changamoto nyingi na tofauti tofauti wanazokutana nazo wananchi katika maeneo wanayomiliki.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Kodi kutoka Wizara ya Ardhi Makao makuu Dodoma,Denis Masami amesema, jukumu la msingi la wizara ni kupanga na kupima, lakini hakuna upangaji wala upimaji utakaokuwa na tija kama wananchi watakuwa hawana elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kupimiwa na kupangiwa maeneo yao.

Masami amesema kwamba, elimu inayotolewa sasa nyumba kwa nyumba ni fursa nzuri ya kuboresha kumbukumbu za wamiliki kutokana na uhalisia kwamba wizara imeboresha taratibu nyingi za utoaji huduma zikiwemo zile za ukadiriaji kodi ya pango la ardhi na ulipaji ambapo sasa zinafanyika kielektroniki.

Aidha, Zuberi Njola mkazi wa Mtaa wa Negamsi katika Halmashauri ya Mji wa Babati, ambaye alifikiwa na watoa huduma katika mji wake alifurahia zoezi hilo na kuiomba wizara kuwafikia wengi zaidi.

“Huu ni mkakati mzuri, tulio wengi hatuzijui haki zetu za msingi hasa kuhusiana na masuala ya ardhi. Pia migogoro mingi tunaitengeneza wenyewe kwa sababu hatuna uelewa wa mambo. Kutoa elimu nyumba kwa nyumba kama hivi kunaleta faraja kwetu wananchi, tunaiomba wizara iendeleze mkakati huu kwani tukishirikiana hakutakuwa na migogoro,”amesema Zuberi.

Siku ya elimu ya mlipa kodi ya ardhi ni kampeni maalum iliyoanzishwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi ambapo kila siku ya Ijumaa watendaji wa sekta ya ardhi kote nchini hupita nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa kutoa elimu kwa wamiliki wa ardhi kuhusu sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia sekta ya ardhi.