Na Joyce Kasiki,TimesMajira Online. Dodoma
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amezindua kichwa kimoja cha treni kati ya saba vilivyokuwa vinakarabatiwa katika karakana ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), ukarabati ambao umegharimu sh. bilioni 15 za Kitanzania.
Mbali na hilo, Waziri Kamwelwe amesema serikali inatarajia kupokea mabehewa ya reli ya kisasa katika kipindi cha Februari 2021, ambapo pia kipande cha reli hiyo kutoka Dar es Salaam-Morogoro kitakuwa kimekamilika.
Akizungumza jijini hapa jana wakati akizindua kichwa cha treni ya reli ya kati, Waziri huyo amesema hivi sasa vipande vya Dar es Salaam-Morogoro chenye urefu wa kilomita 300 na Morogoro-Makutupora-Singida chenye urefu wa kilomita 422 vinaendelea kujengwa.
Amesema vipande hivyo vya reli ya kisasa vyenye urefu wa kilomita 722, vinajengwa kwa gharama ya sh. bilioni 7.1 na tayari serikali imeshasaini mikataba miwili kwa ajili ya ununuzi wa vichwa vya treni na mabehewa vitakavyoendeshwa kwa umeme.
Kuhusu uzinduzi wa kichwa cha kuvuta mabehewa katika reli ya kati, Mhandisi Kamwelwe amesema serikali inaendelea na ukarabati mkubwa wa reli hiyo kutoka Dar es Salaam-Isaka nchini Zambia yenye urefu wa kilomita 970.
Amesema mradi huo, unatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mkopo wa masharti nafuu na unatekelezwa na mkandarasi kutoka Serikali ya China (China Civilling Consultant Cooperation).
Kwa mujibu wa Waziri huyo, maboresho hayo pia yanahusisha ununuzi wa mabehewa 44 mapya na vichwa vitatu vikubwa, vinatarajiwa kuwasili nchini Desemba mwaka huu na Machi 2021.
More Stories
Rais Samia apeleka Bil. 6 kuboresha sekta ya elimu Kaliua
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo