July 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi zaidi ya 1,000 wapata elimu ya Sheria

Na Joyce Kasiki,Dar

MKURUGENZI Msaidizi wa Sehemu ya Usuluhisho kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Felix Chakila, amesema wizara imeendelea kutumia Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 50  kutoa elimu ya masuala ya sheria na kusogeza huduma karibu na wananchi ili kuwasaidia kupata suluhisho la changamoto mbalimbali za kisheria.

Chakila amesema hayo Julai 7,2026 wakati akizungimza na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya kinataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar Es Salaam .

Alisema tangu kuanza kwa maonesho hayo  28 Juni 2026, wizara imehudumia takribani wananchi 1,300 waliofika katika banda lake kutafuta ushauri na huduma za kisheria.

Alisema miongoni mwa masuala yaliyowasilishwa kwa wingi ni migogoro ya mirathi, mashauri ya jinai, changamoto zinazowahusu wananchi katika taasisi za serikali pamoja na migogoro ya ardhi.

Kwa mujibu wake, baadhi ya wananchi wamepatiwa ushauri wa kisheria moja kwa moja, huku wengine wakielekezwa kwenye mamlaka husika zenye uwezo wa kushughulikia na kutatua changamoto zao kwa mujibu wa sheria.

“Fursa ya kushiriki maoneshoni haya imetuwezesha kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali ya sheria na kuwasaidia wananchi kuelewa haki zao pamoja na taratibu za kupata huduma za kisheria,” amesema Chakila.

Aidha, amewahimiza wananchi kutumia siku zilizobaki za maonesho kufika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria ili kupata huduma za ushauri wa kisheria bila malipo na kutafutiwa ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika jamii.