July 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yakabidhi gari kuboresha afya ya mzazi Mbeya

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya.

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha huduma za afya nchini baada ya kukabidhi gari maalum litakalosaidia kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi.

Akizungumza wakati wa kupokea gari hilo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Mratibu wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto wa Kanda hiyo, Magdalena Swebe, alisema hatua hiyo inaakisi dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha huduma za afya na kuhakikisha wananchi, hususan wajawazito, akina mama na watoto, wanapata huduma bora kwa wakati.

Swebe alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka kipaumbele katika afya ya uzazi salama na ustawi wa mama na mtoto, akisema gari hilo litasaidia kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa huduma za afya hadi ngazi za vituo vya kutolea huduma.

Alieleza kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi wa wataalamu wa afya na kuchangia kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.

“Mafanikio yanayopatikana katika sekta ya afya ya uzazi na mtoto katika ukanda huu ni makubwa.

“Hii inaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuokoa maisha ya wananchi na kuendelea kuboresha huduma za afya nchini,” alisema Swebe.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Myriam Msalale, alisema hospitali hiyo imeendelea kupiga hatua kutokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali, ikiwemo ujenzi wa jengo la kisasa la huduma za afya ya uzazi na watoto wachanga, kuongezeka kwa watumishi wa afya, upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa na kukabidhiwa kwa gari hilo jipya.

Msalale pia alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Dk. Godlove Mbwanji, kwa uongozi wake imara unaosimamia kwa ufanisi utekelezaji wa miradi ya maendeleo na maboresho ya huduma za afya, hatua ambazo zimeendelea kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi.