July 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

GCLA kutumia teknolojia za kisasa kuimarisha huduma

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imesema imeendelea kuimarisha huduma za uchunguzi wa kisayansi na jinai kwa kutumia teknolojia za kisasa pamoja na mifumo ya kidijitali inayorahisisha ufuatiliaji wa sampuli, hatua inayolenga kuongeza ufanisi, uwazi na kasi ya utoaji wa matokeo ya uchunguzi.

Akizungumza Julai 5,2026  kwenye banda la Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kwenye maonyesho ya Kimataifa ya Biashara jijini Dar E Salaam kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai wa GCLA, David Elias, amesema maabara za Mkemia Mkuu wa Serikali hufanya uchunguzi wa aina mbalimbali za sampuli zikiwemo za vyakula, maji, vinywaji, dawa na bidhaa nyingine zinazotumiwa na binadamu.

Amesema maabara hizo zimeidhinishwa kwa viwango vya kimataifa, hali inayofanya matokeo ya uchunguzi yanayotolewa kutambulika na kukubalika ndani na nje ya Tanzania.

“Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika vifaa vya kisasa na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi wa huduma za uchunguzi wa kisayansi, hususan katika uchunguzi wa makosa ya jinai,” amesema Elias.

Amefafanua kuwa kupitia mfumo wa kidijitali, maafisa wanaokusanya sampuli katika maeneo ya matukio wanaweza kuzituma kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi wa kina endapo watakuwa na mashaka kuhusu ushahidi walioupata.

Kwa mujibu wake, mara sampuli inapopokelewa maabara, mhusika anaweza kufuatilia hatua zote za uchunguzi kwa njia ya mtandao, kuanzia kupokelewa kwa sampuli, maendeleo ya uchunguzi hadi matokeo yanapokuwa tayari.

Elias amesema matumizi ya mfumo huo yanalenga kuharakisha uchunguzi wa mashauri mbalimbali, hususan ya jinai, pamoja na kuongeza uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma.

Aidha, amesema GCLA inaendelea kutumia teknolojia za kisasa za uchunguzi wa kisayansi zinazowezesha kubaini wahusika wa uhalifu kwa usahihi kupitia ushahidi wa kisayansi unaokubalika kitaifa na kimataifa.

Amesisitiza kuwa uwekezaji huo unaimarisha mfumo wa haki kwa kuhakikisha ushahidi wa kisayansi unaotolewa ni wa kuaminika na kuwafanya wahalifu washindwe kukwepa mkono wa sheria.

Pia amewahakikishia wananchi na wawekezaji kuwa huduma zote zinazotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali zinazingatia viwango vya kimataifa, huku matokeo ya uchunguzi yakitambulika na kukubalika ndani na nje ya Tanzania.