
Na Mwandishi wetu, TimesmajiraOnline,Mbeya .
VIONGOZI wa vyama vya siasa mkoani Mbeya wamewataka wananchi kuendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano, wakisisitiza kuwa hakuna maandamano yaliyopangwa mkoani humo na kuwataka waendelee na shughuli zao za kila siku bila hofu.
Kauli hiyo imetolewa Julai 6, 2026, katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa vyama vya siasa na uongozi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, kilichoongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, ambapo walijadili masuala ya amani, utulivu na usalama.

Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya, Hamadi Mbeyale, amesema chama chake hakijaratibu wala kuandaa maandamano yoyote, hivyo akawataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida bila wasiwasi.
“Sisi hatujaratibu kuandaa maandamano yoyote. Tunawataka wananchi waendelee kufanya shughuli zao kama kawaida pasipo na shaka yoyote,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Langael Akyoo, amesema viongozi wa vyama vya siasa wamekubaliana kwa kauli moja kuwa hakuna maandamano yaliyopangwa mkoani humo, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea na kazi, biashara na shughuli nyingine za maendeleo bila hofu.

Naye Mwenyekiti wa CHAUMA Mkoa wa Mbeya, Ipyana Samson, amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuwa mabalozi wa amani kwa wafuasi wao na jamii kwa ujumla, huku akisisitiza umuhimu wa kukemea vitendo vya vurugu na maandamano yanayokiuka sheria.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema linaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa raia pamoja na mali zao, na limewahimiza wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

More Stories
Ndejembi ajadili awamu ya pili ya mradi wa umeme wa jua kishapu
Airtel yaweka alama ruaha Marathon 2026
Aliyekuwa Mwenyekiti CHADEMA ahamia CCMÂ