Na Joyce Kasiki,Timemajira online
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu Profesa Palamagamba Kabudi, amewahimiza wananchi kutembelea banda la Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam ili kupata huduma mbalimbali, ushauri na ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.
Akizungumza alipotembelea banda la TAMISEMI, Prof. Kabudi alisema wananchi wanapaswa kutumia maonyesho hayo kama fursa ya kukutana ana kwa ana na wataalamu wa Serikali ili kupata majibu ya changamoto zao.
“Ninawahimiza wananchi wote watembelee banda la TAMISEMI. Hapa wanapata nafasi ya kueleza changamoto zao, kusikilizwa na kupata ushauri pamoja na ufumbuzi wa masuala mbalimbali yanayowahusu,” alisema Prof. Kabudi.
Alisema amefurahishwa na namna wataalamu wa TAMISEMI wanavyotoa huduma kwa wananchi, hususan katika kuwasaidia wanafunzi na wazazi kuhusu uchaguzi wa tahasusi za kidato cha tano.
“Moja ya mambo yaliyonivutia ni kuona vijana wengi waliomaliza kidato cha nne na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano wakipata ushauri kuhusu tahasusi walizopangiwa. Wapo waliokuwa na wasiwasi, lakini wamepata maelekezo yanayowasaidia kufanya maamuzi sahihi kwa kufuata taratibu zilizopo,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Roida Andusamile, alisema banda hilo limekuwa likipokea wanafunzi wengi waliochaguliwa kuingia kidato cha tano pamoja na wazazi wao wanaohitaji ufafanuzi kuhusu tahasusi walizopangiwa.
“Tumekuwa tukipokea wanafunzi wengi na wazazi wao. Tunawapa maelezo kuhusu tahasusi walizochaguliwa na kuwaelekeza pale wanapohitaji ushauri au kufuata taratibu za kufanya marekebisho. Wanaondoka wakiwa wameelewa na kuridhishwa na huduma wanazopata,” alisema Roida.
Aliongeza kuwa TAMISEMI itaendelea kutoa huduma kwa wananchi wote watakaotembelea banda hilo katika kipindi chote cha maonyesho, huku akiwakaribisha wananchi kutumia fursa hiyo kupata ushauri na ufumbuzi wa changamoto mbalimbali.

More Stories
Dkt.Munisi:Mambo mazuri yapo banda la Waziri Mkuu
Mahundi afichua nguzo Muhimu kwa familia imara
Polisi Mbeya yakamata wanachuo wanne kuhamasisha vurugu