July 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

IGP apongeza maendeleo Jeshi la Zimamoto Sabasaba

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online

MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP) Camillus Wambura ametembelea banda la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo amepongeza maendeleo makubwa yaliyofikiwa na jeshi hilo kutokana na uwezeshaji unaotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza mara baada ya kutembelea banda hilo Julai 5,2026, IGP alisema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limepiga hatua kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hususan katika upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kuzima moto na kufanya shughuli za uokoaji.

Alisema hapo awali jeshi hilo lilikuwa na wataalamu wenye uwezo, lakini lilikuwa na changamoto ya upungufu wa vifaa, hali iliyokuwa ikikwamisha utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi.

“Tunaona hatua kubwa imepigwa kwa Jeshi hili tofauti na miaka ya nyuma. Lilikuwa na uwezo mdogo wa vifaa, hata kama kulikuwa na wataalamu, bila vifaa ni kazi bure. Ninafahamu hata wataalamu wameongezeka na sasa mnaenda sambamba na majeshi ya uokoaji,” alisema IGP.

Katika ziara hiyo, IGP alipita katika vitengo mbalimbali vya banda hilo na kujionea vifaa vya kisasa vinavyotumika katika shughuli za uokoaji na zimamoto pamoja na elimu inayotolewa kwa wananchi kuhusu namna ya kukabiliana na majanga.

Katika Kitengo cha Elimu kwa Umma, alipata maelezo kuhusu kampeni za utoaji elimu kwa wananchi juu ya tahadhari na hatua za awali za kujikinga wakati wa majanga mbalimbali ikiwemo moto, mafuriko na kuporomoka kwa majengo.

Maafisa wa kitengo hicho walieleza kuwa wananchi hufundishwa kuwa endapo moto utatokea ndani ya jengo, hatua ya awali ya kujinusuru ni kulala chini ili kupata hewa safi, kwa kuwa moshi mzito na hewa chafu hupanda juu.

Aidha, wananchi hupewa elimu ya namna ya kujikinga wakati wa kuporomoka kwa majengo kwa kuelekezwa kukimbilia karibu na nguzo imara au kwenye kona za jengo ambazo zinaweza kutoa nafasi salama zaidi ya kujinusuru.

IGP pia alitembelea Kitengo cha Vifaa vya Uokoaji, ambapo alijionea vifaa mbalimbali vya kisasa  vinavyotumika katika shughuli za uokoaji na kusikiliza maelezo kuhusu namna wananchi wanavyofundishwa matumizi sahihi ya baadhi ya vifaa hivyo katika kukabiliana na dharura.

Alihitimisha ziara yake kwa kuwapongeza viongozi na askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuokoa maisha na mali za wananchi pamoja na kuendelea kutoa elimu ya kinga dhidi ya majanga, akisisitiza kuwa uwekezaji unaofanywa na Serikali umeongeza uwezo wa jeshi hilo kuhudumia wananchi kwa ufanisi zaidi