July 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANOIL  kupanua biashara kwa bidhaa mpya ya  LPG

Na Joyce Kasiki, Times Majira


KAMPUNI Tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), TANOIL, imejipanga  kupanua wigo wa biashara zake kwa kuanzisha bidhaa mpya ya gesi ya kupikia (LPG) pamoja na vilainishi (lubricants), hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa bidhaa za nishati na kuimarisha huduma kwa wateja nchini.

Akizungumza Julai 3,2026  na waandishi wa habari katika banda la TPDC kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa Masoko wa TANOIL, Grace Chigugu, alisema kwa sasa kampuni hiyo inaendelea na shughuli za uuzaji wa mafuta ya petroli na dizeli kwa mfumo wa jumla  kwa kampuni za uuzaji wa mafuta , huku ikikamilisha maandalizi ya kuingiza sokoni bidhaa ya LPG.

Alisema taratibu zote muhimu za kuanzisha biashara ya gesi ya kupikia zimefikia hatua za mwisho na mara bidhaa hiyo itakapoanza kupatikana sokoni, TANOIL itakuwa tayari kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na bidhaa zenye ubora unaotakiwa.

“Tunawaalika wamiliki wa vituo vya mafuta, wasambazaji wa gesi, viwanda, migodi, wakandarasi na wadau wengine wa sekta ya nishati kushirikiana na TANOIL katika kusambaza na kutumia bidhaa zetu. Lengo letu ni kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika na yenye ubora wakati wote,” alisema Chigugu.

Aliongeza kuwa mbali na LPG, kampuni hiyo pia ina mpango wa kuanza kuuza vilainishi (lubricants), hatua itakayopanua huduma zake na kuongeza chaguzi kwa wateja wa sekta mbalimbali za uchumi.

Kwa mujibu wa Chigugu, TANOIL imejipanga kutoa huduma bora kwa kuhakikisha mafuta na bidhaa nyingine zinawafikia wateja kwa wakati, huku ikijenga ushirikiano wa muda mrefu unaozingatia mahitaji ya wateja hata katika nyakati za changamoto za upatikanaji wa mafuta.

Alisema kutokana na kuwa kampuni ya Serikali, TANOIL ina jukumu la kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta wakati wote ili kuimarisha usalama wa nishati na kuendelea kuchochea shughuli za uzalishaji na maendeleo ya kiuchumi.

Aidha, aliwahimiza wamiliki wa vituo vya mafuta, wadogo, wa kati na wakubwa, kutumia fursa ya kushirikiana na TANOIL kwa kuwa kampuni hiyo ina mifumo rafiki ya biashara ikiwemo malipo ya fedha taslimu na mikopo inayowawezesha kukuza biashara zao.

Kwa upande wa viwanda, migodi na wakandarasi, alisema TANOIL imejipanga kuhakikisha wanapata mafuta kwa wakati ili shughuli zao za uzalishaji zisiathiriwe na changamoto za upatikanaji wa nishati.

“TANOIL imejikita katika kutoa huduma za uhakika, bidhaa zenye ubora na ushirikiano wa kudumu kwa wateja wake. Tunawaalika wadau wote kushirikiana nasi katika safari hii ya kupanua huduma na kuchangia maendeleo ya sekta ya nishati nchini,” alisema Chigugu.