Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameipongeza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa hatua kubwa ilizopiga katika matumizi ya teknolojia za kidijitali na uboreshaji wa huduma zake kwa wananchi.
Kapinga alitoa pongezi hizo Julai 1, 2026, alipotembelea banda la TEMESA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama Sabasaba, yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika banda hilo, Waziri Kapinga alipata fursa ya kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na wakala huo, ikiwemo matengenezo ya magari na mitambo, huduma za vivuko, umeme na elektroniki, ushauri wa kihandisi pamoja na mifumo ya kidijitali inayorahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Nawapongeza TEMESA kwa kazi nzuri mnayofanya. Mabadiliko yanayoonekana katika utoaji huduma na matumizi ya mifumo ya kidijitali yanaonesha dhamira ya taasisi hii ya kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya wananchi,” alisema Kapinga.
Alisema maboresho hayo yana mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi, kupunguza gharama za huduma na kuimarisha utoaji wa huduma za umma kwa viwango vinavyokidhi matarajio ya wananchi.

Kwa upande wake, TEMESA imeendelea kutumia maonesho hayo kuelezea shughuli zake na mafanikio yaliyopatikana katika sekta za ufundi, umeme na usafiri, huku ikiwahamasisha wananchi na wadau kutembelea banda lake ili kupata taarifa na ushauri wa kitaalamu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na wakala huo.
Maonesho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu ya “Hii ni Kubwa Kuliko” na yanatarajiwa kufunguliwa rasmi Julai 3, 2026. TEMESA ni miongoni mwa taasisi zinazotumia maonesho hayo kuonesha mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini kupitia huduma za ufundi na uhandisi.

More Stories
TOSCI Yahimiza Matumizi ya Mbegu Zilizohakikiwa
Wanawake wanufaika zaidi ya Asilimia 51 mikopo SELF
Waziri apongeza NBS kuweka Takwimu Mtandaoni