July 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri ahimiza Wananchi kutumia huduma Sabasaba



Na Joyce Kasiki, Times Majira


WAZIRI wa Katiba na Sheria Dkt.Juma Homera ametembelea banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam na kuwataka wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kupata huduma mbalimbali za kisheria na usajili kwa haraka, ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, ndoa na vifo ndani ya saa 48.


Akizungumza mara baada ya kutembelea banda hilo Julai 3,2026 Waziri alisema Wizara ya Katiba na Sheria inahudumia maisha ya mwananchi kuanzia kuzaliwa hadi kufariki dunia kupitia taasisi zake mbalimbali zinazotoa huduma za usajili na msaada wa kisheria.


Alisema wananchi wanaohitaji vyeti vya kuzaliwa, ndoa au vifo wanapaswa kutembelea banda la wizara hiyo ambapo huduma hizo zinapatikana kwa urahisi, huku akibainisha kuwa serikali imezindua mfumo unaowezesha vyeti hivyo kutolewa ndani ya saa 48 baada ya kukamilika kwa usajili.


“Tunawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kutembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria. Hapa ndipo mahali pa kupata msaada wa kisheria, ushauri wa kitaalamu na huduma mbalimbali zinazohusu haki na sheria,” alisema Waziri.


Aidha, alisema wananchi wanaokabiliwa na changamoto za kisheria wanaweza kupata msaada wa mawakili pamoja na ushauri unaotolewa kupitia taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa haki kwa wote.


Kuhusu mchango wa Wizara ya Katiba na Sheria katika maendeleo ya taifa, Waziri alisema wizara hiyo ni mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi kwa kuwa sheria bora zimeendelea kuweka mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji nchini.


Alieleza kuwa marekebisho mbalimbali ya sheria yamefanyika ili kurahisisha uwekezaji, usajili wa kampuni na shughuli nyingine za kiuchumi, jambo ambalo limeongeza imani kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.


Waziri alisema serikali inaendelea kupitia sheria mbalimbali ili ziendane na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kuimarisha utawala bora, haki za binadamu, uwazi, amani, utulivu na maendeleo endelevu.


Alisisitiza kuwa sheria ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa na kuwataka wananchi kuendelea kuziheshimu na kuzifuata, akionya kuwa yeyote atakayekiuka sheria atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.


“Sheria ni maisha yetu na ndiyo moyo wa maendeleo ya Tanzania. Kila mwananchi anapaswa kuilinda na kuitii kwa maslahi ya taifa,” alisema.