Na Joyce Kasiki
Mtaalamu wa Jiolojia kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Magambo Samweli, amesema shirika linaendelea na juhudi za kufanya tafiti za mafuta na gesi nchini kupitia miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Serikali, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la TPDC kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Magambo alisema lengo la ushiriki wa TPDC ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu ya shirika pamoja na maendeleo ya miradi ya utafutaji wa mafuta na gesi.
Alieleza kuwa kwa sasa TPDC inaendelea na mradi wa utafiti katika Bonde la Eyasi, unaohusisha mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Tabora, Singida na Manyara, huku ukitarajiwa kuendelea kuelekea Arusha.
“Kama nilivyoeleza, mradi wa Bonde la Eyasi kwa sasa uko hai. Timu ya wataalamu wa TPDC inaendelea na shughuli za utafutaji wa mafuta. Tafiti zinaonyesha kuwa jiolojia ya eneo hili inafanana na ile ya maeneo ya Uganda ambako mafuta yaligunduliwa, hivyo tuna matumaini makubwa ya kufikia mafanikio,” alisema Magambo.
Alifafanua kuwa hatua inayoendelea sasa ni ukusanyaji wa data za mitetemo ya 2D (2D seismic survey), ambapo wataalamu hutumia teknolojia ya kuchunguza miamba iliyopo chini ya ardhi ili kubaini maeneo yenye uwezo wa kuzalisha na kuhifadhi mafuta au gesi.
Kwa mujibu wake, awamu ya kwanza ya ukusanyaji wa data ilifanyika mwaka 2022 ambapo kilomita takribani 250 za data za mitetemo zilichukuliwa. Hivi sasa TPDC ipo katika awamu ya pili ya mradi huo, ikikusanya kilomita 1,910 za data za mitetemo kabla ya kuendelea na hatua zinazofuata za uchambuzi.
Magambo alisema mradi huo unafadhiliwa kwa fedha za ndani zinazotolewa na Serikali kupitia TPDC, ikiwa ni mkakati wa kupunguza gharama za utafiti pale wawekezaji watakaposhirikishwa katika hatua zinazofuata za maendeleo ya miradi ya mafuta na gesi.
Mbali na Bonde la Eyasi, alisema TPDC pia inaendelea na maandalizi ya kuanza utafiti katika kitalu cha Songo Songo Mashariki, ambapo ukusanyaji wa data za mitetemo unatarajiwa kuanza mwaka ujao baada ya bajeti ya mradi huo kuidhinishwa.
Alisema eneo hilo lina matarajio makubwa kutokana na ukaribu wake na kitalu cha Songo Songo kinachozalisha gesi asilia inayosafirishwa kupitia bomba kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
“Lengo la Serikali ni kuendelea kuwekeza katika tafiti za mafuta na gesi ili kuongeza fursa za ugunduzi wa rasilimali hizi. Hadi sasa TPDC imefanikiwa kugundua gesi asilia, lakini bado tunaendelea na jitihada za kugundua mafuta, hususan katika Bonde la Eyasi,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka kwa ajili ya shughuli za utafiti wa mafuta na gesi kupitia TPDC, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa nishati, kuvutia uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia sekta ya petroli.

More Stories
Fkt:Mambo mazuri yapo banda la Waziri Mkuu
Mahundi afichua nguzo Muhimu kwa familia imara
Polisi Mbeya yakamata wanachuo wanne kuhamasisha vurugu