Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
VIJANA wametakiwa kumkumbuka na kumtanguliza Mungu wakiwa katika umri wa ujana,kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuharibu maisha yao na kutumia fursa walizonazo kuleta mabadiliko chanya katika jamii na Taifa.
Wito huo umetolewa na Julai 1,2026 na Mwenyekiti wa Vijana wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Usharika wa Makedonia Mjimwema, wilayani Ilemela mkoani Mwanza Eliud Paul,wakati akizungumzia na Majira kanisani hapo,ambapo alisema mwishoni mwa wiki jana usharika huo uliadhimisha wiki ya vijana ambayo yaliwapa vijana fursa ya kushiriki shughuli mbalimbali zilizolenga kuwajenga kiroho na kijamii.
Akirejea maandiko matakatifu kutoka kitabu cha Mhubiri 12:1, Paul alinukuu, “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijaja siku zilizo mbaya, wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo,”.Alisema, andiko hilo linawakumbusha vijana kumkumbuka Mungu katika maisha yao, hasa wakati huu ambapo wengi wanapitia changamoto mbalimbali zinazoweza kuleta madhara makubwa kwao na kwa jamii.
Amesema maandiko hayo pia yanawakumbusha vijana kutumia nafasi waliyonayo kufanya mambo yenye kuleta mabadiliko chanya katika jamii na Taifa, kwa kuwa wao ndio nguvu kubwa ya maendeleo.Hivyo aliwataka kumtumikia Mungu, kufanya yanayompendeza na kuachana na vitendo vinavyoweza kusababisha madhara makubwa katika maisha yao.
Aidha amesema,vijana wana wajibu wa kusimamia na kuendeleza amani katika taifa na katika maeneo wanayoishi kwa kuepuka njia zinazoweza kuharibu maisha yao.Aliwasihi vijana wa kanisa hilo na jamii kwa ujumla kumrudia Mungu, kutumia vyema fursa zilizopo na kuwa chachu ya maendeleo kwa manufaa ya taifa.
“Tukijitambua katika nafasi zetu tuna uwezo wa kufanya mambo makubwa na jamii ikatutazama kwa jicho la pili,”amesema Paul.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Msaidizi wa Vijana wa KKKT Usharika wa Makedonia Mjimwema, Kemirembe Kennedy,amewasisitiza mabinti kuwajibika katika kumtumikia Mungu kupitia shughuli za kanisa na za kijamii.Huku akiwahimiza kuwa na msimamo,kujitambua,kujisimamia na kutoruhusu changamoto za kijamii, makundi au vishawishi kuwazuia kutimiza maono na malengo waliyojiwekea.
Amesema mabinti wana nafasi kubwa katika jamii na kanisa ya kuwezesha maendeleo kwa kumtanguliza Mungu na kutumia fursa walizonazo, ikiwemo kujishughulisha na kazi za mikono na shughuli nyingine zenye tija, huku wakiepuka vishawishi vinavyoweza kuathiri ndoto zao.
Naye mmoja wa vijana wa usharika huo, Japhet Johnston,amesema maadhimisho ya Wiki ya Vijana yaliendeshwa kwa kaulimbiu isemayo, “Kanisa ni msingi wa malezi bora.” Akirejea maandiko kutoka 1 Timotheo 4:12,”Mtu awaye yote asiudharau ujana wako,bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo,na katika upendo na imani na usafi,”.
Kupitia neno hilo Johnston amesema,vijana wanapaswa kubadili mwenendo wao na kuwa mfano wa matendo mema ili jamii iwaamini na waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazojitokeza. Aidha, alitoa wito kwa wazazi na walezi kuendelea kuwafundisha, kuwalea na kuwaelekeza vijana katika misingi ya maadili na hofu ya Mungu.

More Stories
Balozi Omar apongeza Juhudi za kulinda amana za wateja
Tani 22.6 dawa za kulevya zakamatwa, 188 wanaswa
BRELA yaelekezwa kuwasaidia Wafanyabiashara maonesho ya Sabasaba