Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
WATUMISHI wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza,wametakiwa kuhakikisha wanafuata taratibu za utumishi wa umma ili kuepuka adhabu mbalimbali pindi watakapozikiuka taratibu hizo.
Wito huo umetolewa Julai 1,2026 na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma,Salama Twalibu,wakati walipotoa elimu kwa Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela juu ya kazi za Tume hiyo sambamba na kukumbushwa juu ya haki na wajibu wao katika utumishi wa umma.

Ambapo elimu hiyo imetolewa na Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma kupitia viongozi waliofika katika halmshauri hiyo kwa lengo la kuitambulisha tume kwa watumishi wa umma pamoja na kusikiliza masuala yoyote yanayowatatiza kuhusu sheria,taratibu na kanuni pamoja na kuwakumbusha juu ya wajibu na haki zao katika nchi.
Twalibu ametolea mfano kukithiri kwa suala la utoro kwa watumishi wa umma ambalo limekuwa likiwasababishia watumishi wengi kujikuta wanachukuliwa hatua za kinidhamu.
Katibu Msaidizi Idara ya Rufaa na Malalamiko kutoka Tume ya Utumishi wa Umma Robert John,amesema kuwa wajibu ni majukumu,kazi na mambo ambayo mtumishi wa umma anatakiwa kutekeleza kwa mujibu wa sheria,kanuni, taratibu na maelekezo ya Serikali pamoja na maadili ya Utumishi wa Umma ili kutoa huduma bora kwa wananchi na kulinda maslahi ya umma.
Huku akisisitiza kuwa haki ni kile Mtumishi wa Umma anatakiwa kufanyiwa na mwajiri lakini wajibu ni kile ambacho mtumishi anapaswa kutimiza.
“Mtumishi wa umma anatakiwa kutimiza wajibu wake kulingana na nafasi na kazi yake aliyonayo kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu.Kutotekeleza wajibu kunaweza kusababisha kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kupewa onyo, kukatwa mshahara, kushushwa cheo au kufukuzwa kazi kulingana na uzito wa kosa husika,”amesema John.

Akiwasilisha mada juu ya kazi na muundo wa Tume ya Utumishi wa Umma, Kamishna wa Tume hiyo Nassor Mnambila amesema,kazi ya tume ni kuhakikisha Utumishi wa Umma unasimamiwa na kuendeshwa kwa mujibu wa sheria taratibu na kanuni.
“Kifungu namba 12 kifungu kidogo cha kwanza kinafafanua namna tume itakavyohakikisha,utumishi wa umma katika nchi yetu unaendeshwa na kusimamiwa kwa mujibu wa sheria.Pia kazi ya tume ni pamoja na kutoa ushauri kwa Rais kulingana na wajibu alio nao chini ya Ibara ya 36 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,urekebu kwa kutoa miongozo sambamba na kutoa elimu kuhusu sera sheria na kanuni za utumishi wa umma,”amesema Mnambila.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Mohammed Atiki amewashukuru viongozi hao wa Tume hiyo kwa elimu waliotoa huku akiahidi kuzingatia na kuyafanyia kazi yale yote ambayo wameelekezwa.


More Stories
Balozi Omar apongeza Juhudi za kulinda amana za wateja
Tani 22.6 dawa za kulevya zakamatwa, 188 wanaswa
BRELA yaelekezwa kuwasaidia Wafanyabiashara maonesho ya Sabasaba