Na Joyce Kasiki
CHUO Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeendelea kupanua programu za masomo na mafunzo ya kitaaluma kwa lengo la kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) katika banda la Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) Afisa Udahili Rahel Mwingo alisema taasisi hiyo kwa sasa inatoa zaidi ya programu 10 za shahada ya kwanza katika fani mbalimbali, ikiwemo elimu, sayansi na taaluma nyingine zinazolenga kuimarisha sekta ya elimu na maendeleo ya jamii.
Amesema mbali na programu za shahada ya kwanza, chuo kinatoa programu 14 za shahada za uzamili pamoja na programu za shahada ya uzamivu (PhD), hatua inayowawezesha wataalamu kuendelea kuongeza ujuzi na kufanya tafiti zenye mchango kwa maendeleo ya nchi.
Aidha, amesema chuo kinafundisha lugha tano ambazo ni Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Kichina na lugha nyingine za kimataifa kwa ngazi za awali, kati na juu, ili kuwawezesha wanafunzi kuhimili ushindani katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Ameongeza kuwa chuo kina shule na vitengo maalumu vya tafiti, ubunifu na maendeleo ya teknolojia, sambamba na kufundisha masuala ya mazingira, TEHAMA na uchambuzi wa takwimu, yanayowaandaa wanafunzi kukabiliana na mahitaji ya dunia ya sasa.
Amewataka wananchi kutembelea banda la chuo katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata taarifa za udahili, programu mbalimbali za masomo na fursa zinazotolewa na taasisi hiyo kwa wanafunzi na watafiti.

More Stories
Balozi Omar apongeza Juhudi za kulinda amana za wateja
Tani 22.6 dawa za kulevya zakamatwa, 188 wanaswa
BRELA yaelekezwa kuwasaidia Wafanyabiashara maonesho ya Sabasaba