July 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chuo Morogoro Chahamasisha Walimu Kujiunga mafunzo ya Ufundi

Na Joyce Kasiki

MKUFUNZI  wa Chuo cha Ufundi Stadi Morogoro Ramadhani Msidada, amewahimiza Watanzania, hususan wahitimu wa kidato cha sita na vyuo mbalimbali, kujiunga na chuo hicho kinachotoa mafunzo ya ualimu wa ufundi (mafunzo ya Amali) kuanzia ngazi ya cheti hadi diploma ili kukidhi mahitaji ya walimu wa ufundi nchini.

Akizungumza Julai Mosi,2026 katika maonyesho ya Kimataifa ya Biashara (SABASABA) katika banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi  (VETA)  kuhusu nafasi ya chuo hicho, Msidada alisema Chuo cha Ualimu wa Ufundi Morogoro kinachosimamiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kimejipanga kuandaa walimu wenye umahiri wa kufundisha katika shule za sekondari zenye mkondo wa ufundi, vyuo vya ufundi na taasisi nyingine za mafunzo nchini.

Amesema kuanzishwa kwa shule za sekondari zenye mkondo wa ufundi kufuatia maboresho ya mtaala wa elimu nchini kumeongeza mahitaji ya walimu wa ufundi, jambo lililoifanya chuo hicho kupanua huduma zake za mafunzo ili kukidhi mahitaji hayo.

Aidha, ameeleza kuwa chuo kimekuwa kikitoa mafunzo ya muda mfupi kwa walimu waliopo kazini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ambapo zaidi ya walimu 100 wamewezeshwa kupata ujuzi wa ufundi kwa ajili ya kuboresha uwezo wao wa kufundisha katika shule za sekondari.

Ramadhani amesema chuo kinaendelea kupokea wanafunzi wapya katika programu za cheti na diploma, huku wanafunzi wanaokidhi vigezo wakipata fursa ya mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, jambo linalowarahisishia kugharamia masomo yao.

Ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha Watanzania wote wenye sifa kujiunga na Chuo cha Ualimu wa Ufundi Morogoro ili kuchangia upatikanaji wa walimu wa ufundi wenye uwezo wa kuimarisha elimu ya ufundi na maendeleo ya Taifa.