June 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenge wa Uhuru ulivyotembelea miradi ya bil.3.6/- Korogwe TC

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

MWENGE wa Uhuru kwa mwaka 2026 uliweza kufika Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga Juni 24, 2026 na kuweza kutembelea miradi ya maendeleo sita yenye thamani ya sh. bilioni 3.6. Miradi hiyo ipo ya afya, elimu, barabara, ukopeshaji wa vikundi vya vijana, na uwekezaji wa hoteli.

Mwandishi wa makala haya alizungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe (TD) , Zahara Msangi, na kuweza kuelezea ufanisi wa miradi hiyo kwa maendeleo ya watumishi hasa kwenye kupata nyumba za kuishi, wananchi na wanafunzi. Lakini pia kwa vijana kuweza kupata mikopo ile ya asilimia 10 kutoka halmashauri kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Wazo Mwang’onda akiweka Jiwe la Msingi ujenzi wa Barabara ya Halmashauri mjini Korogwe.”

Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri ilipanga kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba ya watumishi (two in one) katika Zahanati ya Lwengera Darajani kwa gharama ya sh. 92,780,000 kupitia Mapato ya ndani. Mradi huo ulianza kwa nguvu za wananchi na hatimaye kuendelezwa na Halmashauri, ambapo mwaka 2025 mradi ulipitiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru na uliwekewa jiwe la msingi.

Lengo la Mradi huo ni kuboresha mazingira mazuri ya kufanyia kazi kwa watumishi wa vituo vya kutolea huduma za afya na hatimaye kuboresha huduma za afya kwa ujumla.

“Mradi huu unatekelezwa kwa njia ya “Force Account”. Aidha, jumla ya sh. 92,780,000 zimepokelewa ambapo sh. milioni 82 ni fedha za Mapato ya ndani ya Halmashauri, sh. milioni sita ni fedha za Mfuko wa Jimbo, sh. 3,716,000 ni kutoka kwa Wadau na sh. 1,064,000 ni nguvu za wananchi. Hadi sasa Mradi huu umekamilika kwa asilimia 100 na unatumika.

“Nyumba ya watumishi (two in one), Zahanati ya Lwengera Darajani.”

“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta hii muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu. Pia, tunawashukuru wananchi wa mtaa wa Lwengera Darajani kwa kujitokeza kuchangia utekelezaji wa mradi huu kupitia nguvu kazi na michango ya fedha, Ushirikiano wao umeonesha uzalendo, umoja na ari ya maendeleo” anasema Msangi.

KIKUNDI CHA VIJANA WA MAGUTA

Kikundi cha Vijana cha Maguta Mkuyuni Safari (KIMAMSA) kilianzishwa Oktoba 7, 2024 kikiwa na wanachama watano wote ni wanaume. Kikundi hicho kipo katika Kata ya Manundu na kinafanya shughuli za usafirishaji wa mizigo kwa kutumia Maguta. Kikundi kilianza na mtaji wa sh. milioni 14 ambazo zilipatikana kwa kuchangishana wanakikundi wenyewe.

Lengo la kikundi ni kuboresha shughuli za usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya Halmashauri ya Mji Korogwe na kuboresha Uchumi wa wanakikundi na jamii kwa kujiajiri wenyewe na kuajiri vijana wengine.

Kikundi hicho Agosti 7, 2025, Halmashauri ya Mji Korogwe kiliwakopesha sh. milioni 29.4 kupitia asilimia nne (4) ya vijana itokanayo na makusanyo ya mapato ya ndani. Kupitia mkopo huo wameweza kununua maguta matano. Mkopo huo ni wa muda wa miezi 24 kuanzia Novemba 7, 2025 hadi Oktoba 7, 2027, na kiasi cha rejesho kwa mwezi ni sh. 1,225,000. Mpaka sasa wamerejesha sh. 14,787,500.

“Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwang’onda akitoa somo kwa vijana wa Maguta. Kulia ni Mkurugenzi Korogwe TC, Zahara Msangi.”

Mradi huo umeleta manufaa makubwa kwa wanakikundi na jamii ya Korogwe kwa ujumla kwa kuweza kurahisisha huduma ya usafirishaji wa mizigo katika Mji wa Korogwe. Mtaji wa kikundi kwa sasa umeongezeka kutoka sh. milioni 14 hadi sh. milioni 43.4. Na wameweza kutoa ajira za muda kwa vijana watano watano ambao ni wasaidizi wabeba mizigo wakati wa utoaji wa huduma.

Na vijana hao wanamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia mikopo na uimarishaji wa mazingira ya ujasiriamali. Pia, wameishukuru Halmashauri ya Mji Korogwe kwa kuendelea kuwasimamia na kuwaamini vijana katika kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii

MRADI WA MATENGENEZO YA BARABARA

Mradi wa Matengenezo ya Barabara kwa kiwango cha lami barabara ya Halmashauri ya urefu wa mita 600 kupitia fedha za Mfuko wa Jimbo. Ulianza Agosti 24 2024 na awali ulitarajiwa kukamilika Agosti 27, 2025 lakini kutokana na kucheleweshwa kuondolewa kwa miundombinu ya maji na hali ya hewa ya mvua nyingi. Mkandarasi aliongezewa muda hadi kufikia Julai 30, 2026. Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Ujenzi ya Riso Business Holding Company Limited, ya DODOMA kwa gharama ya sh. milioni 475 bila VAT.

Chanzo cha fedha hizo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mfuko wa Jimbo. Hadi sasa Mkandarasi amelipwa malipo ya sh. 155,316,240 ambazo ni pamoja na kazi za matengenezo ya sehemu korofi na mradi umefikia asilimia 95 ya utekelezaji.

“Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwang’onda akiweka Jiwe la Msingi ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, Shule ya Sekondari Ngombezi.”

Hadi kukamilika kwa mradi huo kazi zinazotarajiwa kufanyika ni kusafisha na kung’oa miti, uhamishaji wa miundombinu ya maji, umeme na simu, kuondoa makalavati yaliyokuwepo mistari mitatu, kuondoa tabaka la udongo usiofaa mita za ujazo 3,200, kujaza changarawe na kushindilia matabaka matatu yenye mita za ujazo 1,980, kuleta, kusambaza na kushindilia kokoto za msingi wa barabara (CRS) mita za ujazo 540, kuweka lami nyepesi mc30 mita za eneo 4200, kuweka lami tabaka la kwanza na la pili mita za eneo 8400, kuweka alama za barabarani nne (4) na taa nne (4), kujenga mitaro mita za eneo 1500, kujaza mawe mita za ujazo 400

Mradi huo utawanufaisha wananchi katika kufikia huduma za kijamii kama vile elimu, maji na kurahisisha usafiri wa watu kutoka eneo moja kwenda eneo jingine. Mradi huo utaongeza thamani ya maeneo husika na mradi kwa kuwa maeneo hayo yatakuwa yanafikika kwa urahisi majira yote ya mwaka.

UJENZI WA VYUMBA VIWILI VYA MADARQSA NA OFISI YA WALIMU

Shule ya Sekondari Ngombezi ni mojawapo ya shule itakayokabiliwa na ongezeko la wanafunzi double cohort 2028. Shule hiyo inatarajia kupokea jumla ya wanafunzi 243, hivyo basi itakuwa na upungufu wa madarasa manane (8) ambapo Halmashauri ya mji wa Korogwe meanza ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa.

Mradi huo unatarajiwa kutumia jumla ya sh. milioni 50, ambapo hadi sasa fedha iliyopokelewa ni sh. milioni 29.7. Chanzo cha fedha za mradi ni mapato ya ndani ya Halmashauri.

Mradi huo unatekelezwa kwa njia ya force account. Mradi upo kwenye hatua za ukamilishaji sawa na asilimia 78. Fedha zilizotumika hadi sasa ni sh. milioni 29.7.

“Barabara yenye urefu wa mita 600 kutoka HTM hadi Halmashauri ya Mji Korogwe, ujenzi wake ukiwa umefikia asilimia 95.”

“Kwa niaba ya Halmashauri ya Mji Korogwe tunamshukuru kwa dhati Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia chini ya kauli mbiu ya mwenge 2026 isemayo “Tanzania ni Yetu Sote, Tushimane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo” anasema Msangi.

UJENZI CHUMBA CHA DARASA SHULE YA MSINGI MATONDORO

Mradi huo ulianza Oktoba 2025 kwa nguvu za wananchi na baadaye uliendelezwa na Halmashauri ya Mji Korogwe. Wananchi walihamasishwa kuanza ujenzi wa darasa ambapo walishiriki kwa kusafisha eneo la mradi, kusomba mawe na kuchimba msingi ambayo ni thamani yake ni sawa na sh. milioni 2.5.

Lengo la mradi huo ni kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na pia kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa ili kuwezesha mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia na hatimaye kuongeza ufaulu katika shule hiyo.

Mradi huo unatekelezwa kwa njia ya force account. Mradi upo kwenye hatua za ukamilishaji sawa na asilimia 75 ya ujenzi, kazi ambazo hazijafanyika ni ufungaji wa umeme, madirisha, uwekaji wa marumaru na utengenezaji wa madawati.

“Jengo la Mgahawa wa Uzunguni City Park.”

“Mradi huu unatarajiwa kutumia jumla ya sh. milioni 25, ambapo hadi sasa fedha iliyotumika ni sh. milioni 19, ambapo kati ya fedha hizo, sh. milioni 12.5 ni fedha za Serikali Kuu, sh. milioni nne (4) ni fedha za Mfuko wa Jimbo, na sh. milioni 2.5 ni nguvu za wananchi. Kwa mwaka 2026/27 Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani imetenga sh. milioni sita kwa ajili ya kukamilisha Mradi huu” anasema Msangi.

MRADI WA HOTELI YA UZUNGUNI

kampuni ya Uzunguni City Park imeanzishwa mwaka 2025 na inajihusisha na utoaji wa huduma za chakula, vinywaji na malazi kwa wageni na wenyeji ya Wilaya ya Korogwe. Mradi huo una jumla ya majengo tisa ambayo majengo matatu ni ya ghorofa, majengo mawili ni vyumba vya kulala wageni, jengo moja ni ofisi na ukumbi wa mikutano. Majengo mengine ni sehemu ya Bar, Mgahawa, Supermarket, Gym, Saluni ya kiume na kike, majiko ya kisasa ya kupikia vyakula mbalimbali na kumbi za mikutano na sherehe. Kampuni ya UZUNGUNI CITY PARK inaendeshwa kisheria na ina usajili BRELA Na. 403570.

Lengo la kampuni hiyo ni kutoa huduma bora ya chakula, vinywaji na malazi zinazoridhisha kutoa ajira kwa jamii hasa wale walio maeneo ya karibu na kampuni, kukuza na kupanua biashara kwa kuongeza huduma muhimu za kijamii kama vile Saluni ya kiume na kike, Masaji, Swimming pool, Michezo ya Watoto na Huduma ya kuosha magari.

Mradi huo umeanza kukarabatiwa mwaka 2024/25 na bado ukarabati unaendelea kwa njia ya mkandarasi. Aidha, huduma zilizokusudiwa zinaendelea kutolewa kwa kuwa majengo yaliyopo yanakidhi mahitaji ya huduma zilizokusudiwa. Hadi kukamilisha ukarabati mradi unatarajiwa kutumia sh. bilioni tatu.

kampuni imeweza kutoa ajira kwa watumishi 50 wakiwemo wanaume 19 na wanawake 31, ambapo wafanyakazi 46 huingia asubuhi hadi jioni na wengine wanne (4) huingia jioni hadi asubuhi kwa kuwa kituo kinatoa huduma kwa masaa 24.

“Vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu, Shule ya Sekondari Ngombezi.”