Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yamefunguliwa rasmi huku Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) ikiwahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kutumia fursa mbalimbali za biashara, uwekezaji, ubunifu na ajira zilizopo katika maonesho hayo ya kihistoria.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi iliyokwenda sambamba na maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu ya Sabasaba katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere usiku wa kuamkia Juni 28, 2026, Mkurugenzi wa TANTRADE, Dkt. Ratifa Khamis, amesema kufikiwa kwa miaka 50 ni hatua muhimu katika historia ya maonesho hayo, akieleza kuwa yameandaliwa kwa kiwango cha kimataifa na kubeba fursa kwa Watanzania wote.

Amesema kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, wananchi watapata nafasi ya kujifunza, kufanya biashara, kujenga mitandao ya kibiashara, kubadilishana uzoefu na kuona teknolojia pamoja na ubunifu kutoka ndani na nje ya Tanzania.
“Mtanzania yeyote ambaye hatafaidika na fursa zilizopo katika maonesho haya atakuwa amejilaumu mwenyewe,” amesema Dkt. Ratifa.
Amebainisha kuwa Serikali kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuyapa hadhi ya kimataifa maonesho ya Sabasaba, hatua iliyochangia kuongezeka kwa ushiriki wa makampuni kutoka mataifa mbalimbali. Alisema hadi kufikia ufunguzi wa maonesho hayo, kampuni 253 za kimataifa zilikuwa zimethibitisha kushiriki.

Kwa mujibu wa Dkt. Ratifa, maonesho hayo ni jukwaa muhimu kwa wafanyabiashara, wawekezaji, wabunifu, watafiti na wananchi kwa ujumla kujifunza, kupata suluhisho la changamoto mbalimbali, kufungua fursa mpya za uwekezaji na kuongeza ajira.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Bertha Minga, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Sixtus Mapunda, amesema maonesho hayo yanatoa fursa kubwa ya kujenga mitandao ya kibiashara kati ya Watanzania na washiriki kutoka mataifa mbalimbali.

Amewahimiza wananchi kufika mapema katika maonesho hayo ili kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuboresha biashara zao, huku akihakikishia kuwa Serikali imeweka ulinzi na usalama wa kutosha kuhakikisha washiriki wote wanashiriki maonesho hayo katika mazingira salama.

More Stories
Twange afichua kilichosababisha hitilafu ya umeme
Juhudi zasaidia kupunguza uingizwaji bidhaa za magendo
Mwaselela awafariji wafanyabiashara walioathiriwa na moto