Na Mwandishi Wetu, Timesmajira
SERIKALI imezitaka taasisi za umma, washirika wa maendeleo na jamii kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha rasilimali za asili zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kauli hiyo ilitolewa na
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Ally Babu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Uhifadhi wa Bioanuai, Usimamizi Endelevu wa Ardhi na Kuongeza Usalama wa Maji katika Bonde la Ziwa Tanganyika.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Babu amesema mradi huo ni muhimu katika kuimarisha uhifadhi wa bioanuai, matumizi endelevu ya ardhi na ulinzi wa vyanzo vya maji, huku ukichangia kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka Bonde la Ziwa Tanganyika.
Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha shughuli zote za mradi zinatekelezwa kwa wakati, kwa ufanisi na kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa.
“Ni muhimu wadau wote tushirikiane kwa karibu ili kuhakikisha mradi huu unaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Mafanikio yake yatachangia uhifadhi wa mazingira, kuimarisha usalama wa maji na kuboresha ustawi wa wananchi,” amesema Babu.
Ameongeza kuwa Serikali inatarajia kuona kasi kubwa ya utekelezaji wa mradi huo ili manufaa yake yaweze kuwafikia wananchi, hususan wale wanaotegemea rasilimali za Bonde la Ziwa Tanganyika kwa shughuli za kilimo, uvuvi na ufugaji.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Tanganyika, Bona Mremi, amesema mafanikio ya mradi huo yanategemea zaidi uhifadhi wa maeneo ya vyanzo vya maji, hususan Bonde la Mto Malagarasi, ambalo ni chanzo kikuu cha maji yanayoingia Ziwa Tanganyika.
Mremi amesema kuhifadhi Bonde la Malagarasi ni hatua muhimu ya kulinda Ziwa Tanganyika, kwani mito inayopitia katika bonde hilo humwaga maji yake moja kwa moja ziwani.
“Ukihifadhi maeneo ya bonde, maana yake umehifadhi Ziwa Tanganyika, kwa sababu mito inayotiririka katika maeneo hayo huishia Ziwa Tanganyika,” amesema
Amefafanua kuwa mradi huo utanufaisha wananchi wote wanaoishi ndani ya Bonde la Ziwa Tanganyika kupitia kuboreshwa kwa usalama wa maji, uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya ardhi.
Mremi amesema Bonde la Malagarasi limepewa kipaumbele kutokana na ukubwa wake na mchango wake katika mfumo wa ikolojia wa Ziwa Tanganyika.
Ameeleza kuwa bonde hilo lina eneo la takribani kilomita za mraba 67,000 na linakadiriwa kuwa na wakazi wapatao milioni sita, wanaotegemea rasilimali zake kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Amesema kutokana na umuhimu huo, shughuli nyingi za mradi zitaanza katika Bonde la Malagarasi ili kulinda vyanzo vya maji, kupunguza uharibifu wa mazingira na kuhakikisha Ziwa Tanganyika linaendelea kuwa na maji ya kutosha pamoja na bioanuai yake kuhifadhiwa.
Mradi wa Uhifadhi wa Bioanuai, Usimamizi Endelevu wa Ardhi na Kuongeza Usalama wa Maji katika Bonde la Ziwa Tanganyika unalenga kuimarisha uhifadhi wa mazingira, matumizi endelevu ya ardhi na usalama wa maji, huku ukiboresha maisha ya wananchi wanaoishi katika maeneo ya bonde hilo.
Serikali na wadau wa maendeleo wanaamini kuwa utekelezaji wa mradi huo utakuwa chachu ya maendeleo endelevu na utachangia kulinda rasilimali muhimu za Bonde la Ziwa Tanganyika kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

More Stories
Senyamule:Serikali inapaswa kuzitambua Kampuni zinazofanya biashara ya ardhi
Serikali kuendelea kupanua fursa elimu Singida
Kumekucha CDF Cup 2026, NMB yaweka Sh milioni 150