June 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NIRC yatumia wiki ya utumishi kuelimisha

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma

TUME ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imesema miongoni mwa majukumu yake makuu ni kujenga miundombinu mipya ya umwagiliaji, kuchimba mabwawa na visima pamoja na kukarabati miundombinu ya zamani ili kuongeza tija katika sekta ya kilimo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Juni 22,2026 katika banda la Tume hiyo kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa NIRC, Maria Itembe, alisema ushiriki wao katika maadhimisho hayo unalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma na majukumu yanayotekelezwa na taasisi hiyo.

Kwa upande wake, Mhandisi na Mkurugenzi Msaidizi wa Tafiti pamoja na Msimamizi wa Programu ya Uchimbaji wa Visima kutoka NIRC, Naomi Mcharo, amesema programu ya uchimbaji wa visima ni miongoni mwa huduma zinazotolewa na Serikali kwa wananchi, hususan wakulima, ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema kutokana na changamoto za upatikanaji wa maji kwa shughuli za kilimo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliielekeza Tume hiyo kuongeza juhudi za kuwachimbia wananchi visima kwa lengo la kuwawezesha kunufaika na kilimo cha umwagiliaji.

Mhandisi Naomi amesema hadi sasa Tume imefanikiwa kuchimba visima 362 katika mikoa ya Geita, Tabora, Manyara na Singida, ambapo kila kisima kina uwezo wa kuhudumia wastani wa hekari 40 za mashamba ya umwagiliaji.

Aliongeza kuwa mpango wa Tume ni kuhakikisha kila wilaya inapata angalau visima vitano vitakavyowanufaisha wananchi waliopo katika vikundi vya watu 16 kwa kila kisima, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yamekuwa yakitoa fursa kwa taasisi mbalimbali za Serikali kuwasilisha huduma zao kwa wananchi na kupokea maoni yatakayosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.