Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
KUTOKANA na eneo kukua pamoja na kuimarisha usalama wao na mali zao wananchi wa Kata ya Kishiri wilayani Nyamagana mkoani Mwanza wameomba kujengewa kituo cha polisi.
Ombi hilo wamelitoa Juni 20,2026 wakati wa mkutano wa hadhara wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, uliofanyika eneo la Kishiri Kati Kata ya Kishiri.Ambapo mkutano huo ni mwendelezo wa kutoa elimu ya usalama,kusikiliza kero za kiusalama na kuzitatua ili wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo kwa amani.

Mmoja wa wananchi wa eneo hilo,Manura Anthony amesema, changamoto iliopo Kishiri ni kuwa mji umekua hivyo aliomba wajengewe kituo cha polisi.
‘Kata ya Kishiri ilivyokuwa kubwa kiasi hiki yenye idadi ya watu wengi, haina kituo cha polisi? Ninaomba RPC tuwe na kituo cha polisi,”amesema Juma Nkalango, mkazi wa Kishiri.
Akijibu ombi hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbord Mutafungwa,amemuagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya na Mkuu wa Kituo cha Polisi Nyakato kukarabati Kituo cha Polisi Ndofe kilichokuwa kimeharibiwa kwa kuvunjwa vioo huku akisisitiza kuwa ifikapo Juni 22,2026 kituo hicho kianze kutoa huduma kwa wananchi wa Kata hiyo.
DCP.Mutafungwa amewataka wananchi wa Kishiri kujitafakari na kujiepusha na kufanya vitendo vya uhalifu, ikiwemo kuharibu miundombinu ya Serikali.
“Unakwenda kuchoma soko, ofisi ya Mtendaji wa Mtaa, unakwenda kupasua vioo vya kituo cha polisi, unakwenda kuharibu barabara kwa kuchoma matairi, kweli ni jambo zuri hilo?,”amehoji DCP. Mutafungwa.
Sanjari na hayo amesema suala la kuzuia uhalifu siyo la Jeshi la Polisi pekee Bali kila mwananchi anawajibika katika eneo lake,hivyo aliwataka kuwa wazalendo kwa kuipenda na kulinda nchi yao kwa kujiepusha na vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani pamoja na kuishi kwa kufuata sheria za nchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, SSP.Virginia Sodoka, amewashauri uongozi wa Kata ya Kishiri kupitia Mtendaji kukaa na kamati ya usalama ya kata ili kubainisha eneo ambalo watajenga kituo kikubwa cha polisi.
“Mkishatafuta kiwanja, mtakuja Kituo cha Polisi Kati kuonana na mimi kwa ajili ya kupewa ramani na shughuli za ujenzi ziendelee,” amesema SSP.Sodoka.


More Stories
TRA yawagusa watoto njitiÂ
Tanzania yaongeza Wataalamu wa kulinda Amani Kimataifa
Namibia yaenzi historia ya ukombozi Kongwa