June 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wenyeviti wa Vijiji wamlipua Mbunge kunyang’anywa mihuri

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Monduli

MVUTANO mkubwa umeibuka katika Jimbo la Monduli baada ya Mbunge wa Jimbo hilo, Isack Copriano maarufu kama Kadogoo, kutoa kauli bungeni akiunga mkono hatua ya wenyeviti wa vijiji kunyang’anywa mihuri ya Serikali, kauli ambayo imezua hasira na malalamiko kutoka kwa viongozi wa Serikali za Mitaa katika wilaya hiyo.

Wenyeviti hao wanasema kauli ya Mbunge wao imewadhalilisha, imewashushia hadhi mbele ya wananchi na imeondoa imani ya wananchi kwa viongozi waliowachagua kwa kura.

Sintofahamu hiyo ilianza baada ya Mbunge Copriano kuchangia bungeni kuhusu migogoro ya ardhi na matumizi ya mihuri ya Serikali, ambapo alisema wazi kuwa anaunga mkono hatua ya kunyang’anywa kwa wenyeviti wa vijiji mihuri hiyo.

Akizungumza bungeni, Mbunge huyo alisema:
“Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro, na mimi nimefurahi sana na wenyeviti wa vijiji watanisamehe. Niwapongeze sana TAMISEMI kwa kunyang’anya wenyeviti wa vijiji mihuri. Wanyang’anyeni wala msiwarudishie. Kama watanihukumu nayo 2030 wanihukumu nayo.”

Mbunge huyo aliendelea kueleza kuwa baadhi ya wenyeviti wa vijiji wamekuwa wakitumia mihuri hiyo vibaya kwa kushiriki katika ugawaji wa ardhi na maeneo mbalimbali bila kufuata taratibu za kisheria.
“Katika watu wanaochangia kwenye migogoro ya ardhi ni wenyeviti wa vijiji. Unakuta viwanja vinagawanywa, maeneo yanagawanywa bila kufuata utaratibu. Mwenyekiti amegonga pale muhuri. Tamisemi nawapongezeni kwa hiyo na msirudi nyuma, msiwarudishie mihuri hiyo. Wameharibu sana hii nchi,” alisema Copriano.

Mbunge huyo pia alidai kuwa baadhi ya watumishi wa Serikali wamekuwa wakishirikiana na viongozi wa vijiji katika kuruhusu nyaraka zenye mapungufu kupitishwa na kutumika katika masuala ya ardhi.

Alitoa mfano wa nyaraka za mikutano ya vijiji ambazo hazikuwa na saini za wajumbe wala viongozi husika lakini bado zilikuwa zikitumika katika mchakato wa ugawaji wa ardhi na utoaji wa hati za kimila.

Hata hivyo, kauli hiyo imeibua hisia kali kutoka kwa wenyeviti wa vijiji wa Monduli ambao wameitafsiri kuwa ni shambulio dhidi ya viongozi wote wa Serikali za Mitaa nchini.

Katibu wa Wenyeviti wa Vijiji Wilaya ya Monduli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Monduli Mashariki, Joseph Mbilinyi, amesema kauli hiyo imewaumiza sana viongozi wa vijiji kwa sababu imewahukumu wote badala ya kuwachukulia hatua wale wachache wanaoweza kuwa wamekiuka sheria.
“Mimi kama Katibu wa Wenyeviti Wilaya ya Monduli nimelipokea jambo hili kwa masikitiko makubwa mno. Mheshimiwa Mbunge alisimama mbele ya Bunge na kutoa kauli iliyowahusisha wenyeviti wote wa nchi nzima. Kauli hiyo imewaumiza sana viongozi ambao walichaguliwa kwa heshima kubwa na wananchi,” amesema.

Mbilinyi amesema wenyeviti wa vijiji ni viongozi wa Serikali waliopatikana kupitia uchaguzi rasmi uliohusisha wananchi wa maeneo yao na hivyo walitarajia kutetewa badala ya kushutumiwa hadharani.

Amesema hadi kufikia sasa viongozi wengi wameathirika kisaikolojia kutokana na wananchi kuanza kuwatazama kama watu wanaotumia vibaya mihuri ya Serikali.

Kwa mujibu wa Mbilinyi, kikao kilichoitishwa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Gloriana Kimath, kilihudhuriwa na wenyeviti wengi waliokuwa na hofu kuwa huenda walikuwa wanaitwa kukabidhi mihuri yao kutokana na kauli ya Mbunge.

Hata hivyo amesema Mkuu wa Wilaya aliwahakikishia kuwa hakuna mpango wa kunyang’anya mihuri hiyo na kwamba tayari ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi kuhakikisha mihuri hiyo inalindwa kwa mujibu wa sheria.

“Mpaka jana tulifikiri kikao kinachoitwa na DC ni kwenda kutunyang’anya mihuri, lakini tulipofika tukakuta agenda ni tofauti kabisa. Mkuu wa Wilaya alituhakikishia kuwa hakuna jambo kama hilo,” amesema.

Aidha, amesema wenyeviti wa vijiji wa Monduli wametoa msimamo wao wa pamoja wakimtaka Mbunge huyo kuomba radhi hadharani kabla ya kumalizika kwa mkutano wa sasa wa Bunge.

“Tumesema kama Mwenyekiti mmoja amekosea, sheria zipo. Taratibu zipo. Haiwezekani kuwatuhumu wenyeviti wote wa nchi nzima kwa kosa la mtu mmoja. Hilo halikubaliki,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngarash amesema kauli ya Mbunge imewafanya wananchi kuanza kuwatilia shaka viongozi wa vijiji kana kwamba wote wanatumia vibaya mihuri ya Serikali.

Amesema hali hiyo imepunguza heshima yao katika jamii na kuathiri uaminifu waliokuwa nao kwa wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Oldonyolengai, Jeremiah Noah, amesema mihuri ya Serikali ni alama ya mamlaka waliyopewa na wananchi na Serikali, hivyo haiwezi kutumiwa kiholela kama ilivyoelezwa.

Noah amesema maamuzi mengi yanayohitaji matumizi ya mhuri hupitishwa kwanza katika vikao halali vya kijiji kabla ya nyaraka kugongwa muhuri.

“Mhuri haupigwi kwa maamuzi ya Mwenyekiti peke yake. Kuna taratibu za vikao vya kijiji, mashauriano na maamuzi ya wananchi. Ndiyo maana tunahisi tumedhalilishwa sana na kauli hiyo,” amesema.

Ameongeza kuwa kauli ya Mbunge imejenga mazingira ya kutokuaminiana kati ya viongozi wa vijiji na Mbunge wao, jambo ambalo linaweza kuathiri utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao.

Wenyeviti hao sasa wanamtaka Mbunge Isack Joseph Copriano kufuta kauli yake hadharani na kuomba radhi kwa viongozi wa Serikali za Mitaa ambao wanaamini wamefedheheshwa mbele ya wananchi wanaowaongoza.

Wanasema mpaka sasa bado wanasubiri majibu ya Mbunge wao huku wakisisitiza kuwa wanahitaji kurejeshwa kwa heshima yao na kuondolewa kwa taswira kwamba wenyeviti wote wa vijiji nchini wanatumia vibaya mihuri ya Serikali.

Sakata hilo linaendelea kufuatiliwa kwa karibu na wananchi wa Monduli huku wengi wakisubiri kuona kama Mbunge huyo atatoa ufafanuzi zaidi au kusimama na kauli yake aliyoitolea bungeni kwamba wenyeviti wa vijiji wanapaswa kunyang’anywa mihuri kwa maslahi ya kulinda ardhi na rasilimali za wananchi.