June 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kihongosi asimulia magumu aliyopitia, ni kilio na furaha

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Iringa

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amewahimiza wazazi na walezi kote nchini kuzingatia vipaji vya watoto wao tangu wakiwa wadogo ili viweze kukuzwa na kuwa msingi wa mafanikio yao ya baadaye.

Akizungumza katika Shina Na. 10, Tawi la Mafifi, Kata ya Kihesa mjini Iringa, Kihongosi amesema watoto wengi huonyesha dalili za vipaji, uongozi na ubunifu wakiwa katika umri mdogo, hivyo ni wajibu wa wazazi kuvibaini na kuvilea kwa karibu.

Kihongosi ametumia nafasi hiyo kuelezea historia ya maisha yake, akibainisha kuwa alizaliwa na kukulia Kihesa, alisoma Shule ya Msingi Kihesa kabla ya kuendelea na masomo ya sekondari Lugalo na baadaye elimu ya juu.

Amesema katika safari yake ya maisha alipitia changamoto mbalimbali, ikiwemo kufanya biashara ndogondogo, kuendesha bodaboda na ufugaji ili kujikimu na kusaidia gharama za masomo yake.

Aidha, ameeleza kuwa mafanikio aliyoyapata yametokana na bidii, uvumilivu, maombi pamoja na msaada kutoka kwa wazazi, walezi, marafiki na wananchi wa Kihesa ambao waliendelea kumuunga mkono tangu akiwa mdogo.

Kihongosi pia amewasihi vijana kutoruhusu changamoto za maisha kuwakatisha tamaa, akisisitiza kuwa mafanikio yanahitaji juhudi, nidhamu na uthubutu wa kutumia fursa zilizopo kwa ajili ya maendeleo yao.

Aidha, Kihongosi, pia alitembelea na kukagua Mradi wa Shule ya Msingi Nduli na kutoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawalea na kuwafundisha misingi mema watoto wao, ili kuwa na vizazi bora.

Akizungumza na wazazi katika Shule ya Msingi Nduli iliyojengwa kwa thamani ya Sh. Mil 529.5, ukiwa na madarasa 10 ya shule ya msingi, nyumba ya mwalimu, jengo la utawala, matundu 12 ya vyoo katika shule ya msingi, madarasa mawili shule ya awali na matundu ya vyoo sita katika shule ya awali, mradi uliotekelezwa kwa fedha kutoka Serikali kuu.

Kihongosi amesema, watoto ni Taifa la kesho hivyo ni wajibu wa kila mzazi na mlezi kuhakikisha wanawapa malezi bora watoto wao pamoja na kushirikiana na walimu katika masuala ya kitaaluma.

Pia Kihongosi ametoa wito kwa Walimu wa Shule ya Msingi Nduli, kufanya kazi kwa upendo na bidii, akisema kazi ya uwalimu ni miongoni mwa kazi za wito.

Aidha imeelezwa kuwa, lengo la mradi wa ujenzi wa shule hiyo ni kuboresha mazingira ya kujifunzia pamoja na kupunguza msongamano darasani, ambapo imeelezwa kuwa takribani wanafunzi 820 kunufaika na mradi kutoka maeneo ya karibu.