



Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limepongezwa kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, huku likitakiwa kuendelea kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya soko la dunia ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania kimataifa.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga,wakati wa maadhimisho ya kilele cha miaka 50 ya shirika hilo yaliyofanyika katika ofisi zake zilizopo Njedengwa jijini Dodoma, sambamba na uzinduzi wa kitabu kinachoelezea historia, mafanikio na mchango wa taasisi hiyo katika kukuza ubora wa bidhaa na huduma nchini.
Waziri Kapinga amesema TBS imekuwa nguzo muhimu katika kulinda afya na usalama wa wananchi kupitia usimamizi wa viwango vya bidhaa mbalimbali, huku ikichangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta za uzalishaji, biashara na viwanda nchini.
Ameeleza kuwa katika kipindi hiki ambacho dunia inaendelea kubadilika kwa kasi kupitia teknolojia na ubunifu, TBS inapaswa kuwa na dhana ya kujitegemea zaidi kwa kuimarisha mifumo ya kisasa ya utoaji huduma na kuongeza uwezo wake wa kitaalamu ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
“Tunapoadhimisha miaka 50 ya TBS, tunashuhudia mchango mkubwa wa taasisi hii katika kujenga imani ya bidhaa za Tanzania. Hata hivyo, ni muhimu kuendelea kuwekeza katika teknolojia, ubunifu na ushirikiano na sekta binafsi ili kuhakikisha bidhaa zetu zinakidhi viwango vya kimataifa,” amesema Kapinga.
Aidha, Waziri huyo amesisitiza umuhimu wa TBS kuendelea kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi ili kuongeza ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini na kusaidia kutafsiri kwa vitendo maono ya Tanzania ya kuwa taifa lenye uchumi wa viwanda unaozalisha bidhaa zenye ushindani mkubwa katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi,amesema maadhimisho hayo ni fursa ya kutathmini mafanikio yaliyofikiwa na kuweka mikakati mipya ya kuifanya taasisi hiyo kuwa ya kisasa zaidi na yenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto za karne ya 21.
Dkt. Katunzi amesema TBS itaendelea kuimarisha maabara za kisasa, kuongeza matumizi ya teknolojia za kidijitali na kuwekeza katika rasilimali watu ili kuhakikisha huduma za viwango zinakuwa bora zaidi, za haraka na zenye kuaminika.
“TBS inatambua kuwa dunia inabadilika kwa kasi kubwa, huku teknolojia na mazingira ya biashara vikibadilika, hivyo shirika hilo linapaswa kuendelea kuwa imara, bunifu na lenye uwezo wa kujibu changamoto mpya zinazoibuka.”aamesema Dkt. Katunzi
Amebainisha kuwa kwa kipindi cha nusu karne, TBS imekuwa mhimili muhimu wa maendeleo ya viwanda na biashara nchini kwa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na kuuzwa zinazingatia viwango vinavyotakiwa, jambo ambalo limeongeza imani ya walaji na kufungua fursa za biashara katika masoko mbalimbali duniani.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariam Ditopile Mzuzuri, amesema TBS imekuwa mhimili muhimu katika kulinda maslahi ya walaji, kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania na kuchochea ukuaji wa sekta za uzalishaji nchini.
Ditopile amesema ipo haja ya kufanyika kwa mapitio ya kina ya Sera ya Ubora wa Bidhaa ili iweze kuakisi mabadiliko makubwa yaliyotokea katika nyanja za sayansi, teknolojia, biashara na uzalishaji tangu sera hiyo ilipoanzishwa.
“Tunapoipongeza TBS kwa mafanikio ya miaka 50, ni muhimu pia kuangalia mbele na kufanya maboresho yatakayoiwezesha taasisi hii kuendelea kuwa nguzo ya maendeleo ya viwanda, biashara na kilimo katika mazingira ya sasa ya kiteknolojia,” amesema Ditopile.
Ditopile amesema imejijengea rekodi ya kuwa taasisi muhimu katika kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa, kuuzwa na kutumiwa nchini zinakidhi viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya kulinda afya, usalama na maslahi ya watumiaji.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Viwango Afrika (ARSO), Dkt. Hermogene Nsengimana, amesema Julai 2026 Tanzania itakuwa nchi ya saba barani Afrika kupata Alama ya Ubora ya Afrika (Africa Quality Mark) kwenye bidhaa zake.
Amesema kwa hatua hiyo, Tanzania itaungana na Rwanda, Togo, Senegal, Ethiopia, Nigeria na Zimbabwe katika nchi zinazotumia alama hiyo ya ubora inayolenga kuimarisha viwango vya bidhaa barani Afrika.
Amesema Shirikisho la Viwango Afrika limekwisharatibu na kuoanisha takribani viwango 2,600 vinavyolenga sekta za kipaumbele ikiwemo usindikaji wa mazao ya kilimo, sekta ya magari, dawa na bidhaa za afya, usafirishaji na ugavi, pamoja na nguo na bidhaa za ngozi.
Ameeleza kuwa kwa sasa takribani bidhaa 500 katika ngazi ya Afrika zinapitiwa ili kupata Alama ya Ubora ya Afrika, hatua itakayosaidia kurahisisha biashara ndani ya Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Amesema bidhaa za Tanzania ambazo kwa sasa zinabeba alama ya TBS, zitapata fursa ya kuwekewa alama ya ubora ya Afrika, jambo litakaloongeza ushindani na upatikanaji wa masoko katika nchi mbalimbali za bara hilo.

More Stories
JOWUTA yasukuma mwongozo wa kiswahili
Mwinjuma aongoza maelfu washiriki mbio TCB Selous Marathon
Twange awatoa Wananchi hofu kutumia nishati ya umeme katika vyombo vya usafiri