October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya I&M yasheherekea wiki ya huduma kwa wateja

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Oline, Dar es Salaam

BENKI ya I&M Tanzania imeadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja,kwa kutambua mchango muhimu unaotolewa na wafanyakazi wake katika kuwahudumia wateja wao kwa viwango vya juu na kuhakikisha kuwa wanakuwa wenye furaha wakati wote.

Wafanyakazi wa Benki ya I&M wakiwa katika mavazi ya udaktari wakionyesha kuwapatia wateja suluhisho la changamoto za kifedha kwa kuwapatia wateja huduma bora kibenki ili kufanikisha shughuli za kibiashara na uchumi katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yaliofanyika duniani kuanzia Oktoba5 hadi 9, mwaka huu

Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam katika makao makuu ya benki hiyo, ikiambatana na shughuli mbalimbali kwa wateja kama ishara ya shukrani kwa wateja wanaothaminiwa na pia wafanyakazi wake ambao wamekuwa wakitekeleza jukumu muhimu la kutoa huduma bora kwa wateja wakati wote.

Wafanyakazi wa I&M Bank wakisherehekea pamoja na wateja maadhimisho ya wiki ya wateja wafanyakazi wa Benki ya I&M wakiwa katika mavazi ya kitamaduni.

Miongoni mwa shughuli za kusherehesha hafla hiyo na wiki ya huduma kwa wateja zilizofanywa na benki hiyo ni pamoja na maofisa wa juu na waandamizi wa benki hiyo akiwamo Afisa Mtendaji Mkuu, walichukua jukumu la kuhudumia wateja katika matawi mbalimbali kwa siku ya jana.

Sheherehe hiyo ya wiki nzima ni matokeo ya kujitolea kwa benki hiyo ya I&M katika kuongeza ushiriki wa wafanyakazi katika kuunga mkono kaulimbiu ya mwaka huu ya siku hiyo inayosema kuwa, ‘Timu ya ndoto’.

Mbali na ushiriki wa watendaji wakuu, maafisa waandamizi katika kufanya jukumu la huduma kwa wateja, pia wafanyakazi wote wa benki hiyo walipokea barua binafsi za shukurani kwa bidii yao na kujitolea kwao katika kuleta matokeo chanya na furaha kwa wateja katika benki hiyo.

Wafanyakazi wa Benki ya I&M wakiwa wakikata keki katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja

Mkuu wa Mauzo ya rejareja wa benki hiyo,Lilian Mtali alisema katika kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja wanataka onyesha thamani ya watoa huduma kwa wateja.

“Sisi benki ya I&M tunataka kutumia wiki hii ya huduma kwa wateja kuhakikisha kuwa tunawaonyesha thamani na ukarimu wateja wetu,lakini pia kuunga mkono na kutambua kazi nzuri na kubwa inayofanywa na maafisa wa huduma kwa wateja kama dawati namba moja ambalo ni nembo na kilelezo cha huduma bora za benki.

“Kwani sote tunatambua kuwa dawati la huduma kwa wateja ndilo limebeba sura na kilelezo cha huduma bora zinazotolewa na benki, wamekuwa wakaifanyakazi kwa bidi kwani hata pale wateja wanapokuwa na jazba, wao wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha kuwa wanakamilisha mahitaji yao na kuwaacha wakiwa na furaha jambo ambalo ni kipaumbele cha benki,” amesema Lilian.

Wiki ya Huduma kwa Wateja ni maadhimisho ya umuhimu wa huduma kwa wateja na ya watu ambao wanahudumia na kusaidia wateja kila siku.

Hafla hiyo huadhimishwa kila mwaka wakati wa wiki ya kwanza ya Oktoba na wafanyabiashara wote na mashirika yanayolenga huduma kote ulimwenguni, ambayo hutambua umuhimu wa kutoa huduma bora kwa wateja.