June 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

VETA yathibitisha uwezo kwa mhitimu mlemavu

Na Joyce Kasiki, Time Majira Online, Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, ameshangazwa na ubunifu wa mhitimu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Joseph Mtei, mwenye ulemavu, baada ya kumuona akitumia mguu kuchora ramani za majengo kwa njia ya kompyuta.

Ridhiwani alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la VETA katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 jijini Dodoma, ambapo alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na wahitimu wa taasisi hiyo.

Mtei, ambaye amesomea fani ya uchoraji ramani za majengo, kwa sasa ni mwajiriwa wa Kampuni Tanzu ya VETA ya Ujuzi, akijihusisha na ubunifu wa michoro ya majengo pamoja na usanifu wa samani mbalimbali.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mtei alisema licha ya changamoto ya ulemavu aliyo nayo, amekuwa akitumia ujuzi wake kujiajiri na kutoa huduma za usanifu.

“Tuna design samani zote unazoziona hapa, mimi ndiye nimezi-design. Pia tunafanya biashara ya ramani za majengo,” alisema Mtei.

Meneja wa Kampuni Tanzu ya VETA ya Ujuzi, Mhandisi Marco Kapinga, alisema kampuni hiyo imekuwa na dhamira ya kuwaendeleza vijana wakiwemo wenye mahitaji maalum kwa kuwapatia fursa za kujifunza na ajira.

“Mheshimiwa karibu sana,hii ni sehemu ya kuendeleza vijana wakiwemo wenye mahitaji maalum,Joseph amejifunza kwetu na vile vile tumemwajiri kupitia Kampuni ya Ujuzi Company Limited,” alisema Kapinga.

Alisema kampuni hiyo inaendelea kuzalisha bidhaa mbalimbali na kupanua soko lake, ikiwemo kuuza bidhaa za kitalii mkoani Arusha, huku ikijivunia mafanikio baada ya kushinda tuzo ya watengenezaji bora katika maonesho yaliyofanyika Zanzibar.