June 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maofisa Maendeleo waaswa kuelimisha kuhusu Dira 2050

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

WATAALAMU wa Maendeleo ya Jamii, wametakiwa kuhakikisha wanaelimisha wananchi  kuhusu ushiriki wao katika  utekelezaji  wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050,huku wakitumia lugha rahisi ambayo itawezesha mwananchi wa chini hususani vijijini kutambua dira hiyo  ni nini.

Akizungumza Juni 17,2026 wakati akifungua   kongamano na mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha  Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Tanzania(CODEPATA), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana,Dkt. Joel Nanauka,amesema Serikali ipo katika utekekalezaji wa Dira ya 2050,yenye lengo la kujenga taifa jumuishi lenye usawa,haki, mitazamo na fikra chanya.

Hivyo Maofisa Maendeleo ya Jamii wana jukumu muhimu la kuhakikisha jamii inatambua uwezo wao  wa kutumia rasilimali zilizowazunguka kujiletea maendeleo  pamoja na kubadili fikra,mitazamo,mila na desturi  ambazo zinaweza kukwamisha maendeleo.

“Dira ya Taifa 2050 inalenga kujenga jamii yenye fikra chanya, maarifa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku vijana wakipewa nafasi kubwa katika kuleta mabadiliko hayo,”amesema Dkt.Nanauka.

Kwa upande wake Rais wa CODEPATA Victor Kabuje, amesema utekelezaji wa Dira 2050 hauwezi kutegemea miundombinu, uwekezaji katika teknolojia pekee, lazima ujikite pia katika maendeleo ya watu katika jamii.

Ambapo amesisitiza kuwa ili dira hiyo itekelezwe ipasavyo  wananchi wanapaswa  kuelewa vema wapi tumetoka,wapi tulipo? na wapi tunaenda na mtu pekee wa  kuwapa tafsiri rahisi na inayoeleweka kirahisi  ni Mtaalamu wa Maendeleo ya Jamii.

Hivyo Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wana weledi na mbinu ya kuiwezesha jamii kufikia malengo ya dira hiyo ambayo yanahimiza Tanzania tuitakayo 2050 kwa kuwa na Watanzania wenye elimu bora na  ujuzi unaoendana na teknolojia na uchumi wa kisasa.

Jamii yenye afya njema,kipato kizuri na maisha yenye ustawi huku umaskini ukipungua kwa kiwango kikubwa,pia jamii yenye ajira zenye tija na staha au biashara zinazozalisha mapato ya kutosha,inayoishi katika mazingira salama na amani yenye miundombinu bora na huduma za kisasa.Pia yenye usawa wa fursa bila kujali jinsia,umri au kabila na yenye uwezo wa kushiriki katika maendeleo ya taifa na kunufaika na rasilimali za nchi.

“Ili kufikia adhima ya Dira 2050, Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii ni kiungo  baina ya Serikali na Wananchi,kwani wanaendelea kutoa mchango kuhakikisha mafanikio hayo yanaonekana  kupitia uwezeshaji wa jamii kunufaika na huduma zinazotolewa na Serikali na wadau kupitia sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, kilimo, mifugo, uvuvi, maji, mazingira, miundombinu, nishati, ustawi wa jamii, uwezeshaji wa wanawake na vijana kiuchumi pamoja na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia,”amesema Kabuje.