September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaahidi miundombinu bora utoaji huduma za mawasiliano

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Dar

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema Serikali inahakikisha inaweka miundombinu bora, mazingira mazuri ya kiudhibiti katika utoaji wa huduma za mawasiliano kwa ushindani na mfumo madhubuti wa kisheria unaohakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Nne la Mwaka la Tehama lililofanyika Dar es Salaam leo, Kamwelwe amesema miundombinu iliyojengwa nchi nzima imewezesha huduma za mawasiliano kuwafikia wananchi wengi katika maeneo mbalimbali ya nchi na kufanya juhudi kuongezeka zaidi.

“Miundombinu iliyojengwa nchi nzima imewezesha huduma za mawasiliano kuwafikia wananchi wengi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Juhudi hizi zimeongeza idadi ya wananchi wanaotumia intaneti kutoka milioni 3.56 mwaka 2005 hadi kufikia milioni 23 mwaka 2017, idadi ya wenye laini za simu imeongezeka kutoka milioni 2.96 mwaka 2005 hadi kufikia milioni 48 mwezi Machi, mwaka huu 2020,”amesema.
Aidha, amesema juhudi zaidi za pamoja zinahitajika kuhakikisha huduma bora zaidi za mwasiliano zenye intaneti yenye kasi zinawafikia wananchi kwa gharama ambazo wengi wanazimudu ili nao washiriki vizuri katika uchumi unaoendeshwa na TEHAMA (digital economy) bila kikwazo.

Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Nne la Mwaka la Tehama lililofanyika Dar es Salaam leo.

Naye Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Zainabu Chaula, amesema hado sasa asilimia 94 ya mawasiliano yametapakaa nchini na maeneo machache ambayo bado hayajashughulikiwa hasa kutokana na jiografia ya nchi yetu, lakini katika kipindi hiki tutahakikisha tunafikia asilimia 100.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Samson Mwela amesema wametoa vyeti 100 kwa watalamu ili kuweza kusaidia taifa kujua idadi yao na kutambua uwezo wa ndani ya nchi katika masuala ya Tehama