June 12, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana walioshindwa kuripoti JKT wapewa nafasi nyingine

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

VIJANA waliohitimu Kidato cha Sita na kuchaguliwa kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), lakini wakashindwa kuripoti katika makambi waliyopangiwa kutokana na sababu mbalimbali, wametakiwa kuripoti katika makambi ya JKT yaliyo karibu na maeneo wanayoishi kuanzia leo  Juni 12 hadi Juni 15, 2026.

Tamko hilo limetolewa leo Juni 12,2026 na Mkuu wa Tawi la Oparesheni na Mafunzo wa JKT, Brigedia Jenerali Peter Mnyani, kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya JKT, Chamwino mkoani Dodoma kuhusu msisitizo wa wito wa vijana hao.

Brigedia Jenerali Mnyali amesema utaratibu huo umewekwa ili kuwawezesha vijana wote waliochaguliwa kuanza mafunzo yao licha ya changamoto zilizowazuia kufika katika makambi waliyopangiwa awali.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha vijana wote waliopata nafasi ya kujiunga na JKT wanashiriki mafunzo hayo ili waweze kujengewa uzalendo wa kuipenda nchi yao na stadi za maisha.

Hivi karibuni, Meja Jenerali Rajabu Mabele aliwataka vijana waliochaguliwa kuhudhuria mafunzo hayo kwa mujibu wa sheria na kuwahimiza kuripoti katika makambi waliyoelekezwa.

Awali, vijana hao walitakiwa kuripoti kati ya Juni 1 na Juni 7, 2026 muda ambao umeongezwa hadi Juni 15,2026.

“Meja Jenerali Mabele amewataka vijana wote waliochaguliwa na wakashindwa kuripoti katika makambi ya JKT kwa sababu mbalimbali, kwenda kuripoti katika makambi ya JKT yaliyo karibu na maeneo wanayoishi kasoro  Kambi ya Ruvu JKT mkoani Pwani, Makutupora JKT mkoani Dodoma pamoja na Chuo cha Uongozi Kimbiji (CUJKT) kilichopo Kimbiji jijini Dar es Salaam.

JKT imewataka vijana husika kutumia fursa hiyo ya mwisho kuhakikisha wanaripoti kwa wakati ili kuanza mafunzo yao kama ilivyopangwa.