November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BAKWATA yasaka suluhu ya kudumu majanga ya moto

Na Daud Magesa,TimesMajira Online. Mwanza

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza, wamiliki na waendeshaji wa Shule za Kiislamu wamekubaliana kuweka mikakati ya kukakabiliana na majanga ya moto kwenye shule hizo.

Wamiliki hao pia wamependekeza na kuiomba serikali kuwafutia kodi kwenye vifaa vya kubaini viashiria vya moto, kuzima na kudhibiti majanga ya moto kwenye maeneo ya shule ili kuwawezesha kuviagiza nje kwa gharama nafuu kwa sababu hapa nchini vinauzwa kwa bei kubwa.

Makubaliano hayo yamefikiwa juzi baada ya kupokea taarifa ya uongozi wa BAKWATA ya ukaguzi wa miundombinu ya shule zinazomilikiwa na taasisi za kiislamu, iliyobaini kasoro ama upungufu kwenye shule hizo kutokana na kukumbwa na majanga ya moto.

Akisoma taarifa hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA, Shaaban Moshi amesema shule walizotembelea nyingi hazina vifaa vya kubaini viashiria vya moto na vya kuzima moto na zenye vifaa havikidhi, hakuna vituo vya kujiokolea, milango ya kuingia na kutoka mabwenini na miundombinu ya umeme si rafiki, inapotokea ajali ya moto ama dharura.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wamiliki na waendeshaji wa shule hizo wametakiwa kuboresha miundombinu ya majengo, umeme na mengine pamoja na kupata mafunzo ya kukabiliana na majanga ya moto yanapotokea.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Islamic Development Founadation (IDF), Juma Chia almesema liundwe jukwaa la wamiliki wa shule za Kiislamu na wadau wa elimu wakutane kupanga mikakati thabiti ya kumaliza tatizo la moto, wakilitumia jukwaa hilo litasaidia kukabiliana na majanga na changamoto za elimu.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu (JUWAKITA), Amina Masenza ambaye ni Mkuu wa Mkoa mstaafu amesema ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa majanga ya moto, ufanyike ukaguzi wa mifumo ya nyaya za umeme kuona kama imeathiriwa na kutoa elimu ya ushauri nasaha kwa wanafunzi, ili wasishiriki hujuma za moto shuleni.

Akizungumza baada ya taarifa na kupokea mapendekezo ya wadau hao Shekhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Shekhe Hassan Kabeke amesema ukaguzi waliofanya, wamebaini watumishi wa mamlaka za elimu wanatumia lugha isiyofaa na kuchelewa kutoa vibali vya uanzishaji wa mabweni na bodi za shule.