June 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazalishaji teknolojia nishati safi watakiwa kufuata viwango

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOline,Arusha

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wazalishaji wa teknolojia za nishati safi nchini kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi viwango vilivyowekwa ili kulinda afya za watumiaji, mazingira na kuongeza ushindani wa bidhaa hizo katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika maonesho ya teknolojia za nishati safi, mwakilishi wa TBS amesema taasisi hiyo ina jukumu la kutoa leseni na vyeti vya ubora kwa wazalishaji wa majiko banifu pamoja na vifaa vinavyotumika kutengeneza teknolojia hizo ili kuhakikisha vinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Amesema TBS hufanya ukaguzi na upimaji wa malighafi pamoja na bidhaa zilizokamilika kabla ya kupewa vyeti vinavyoruhusu kuingia sokoni, hatua inayolenga kuwajengea watumiaji imani kuwa bidhaa hizo ni salama na zina ubora unaokubalika.

“Tunataka wananchi wawe na uhakika kwamba wanapotumia majiko banifu au teknolojia nyingine za nishati safi wanatumia bidhaa ambazo zimehakikiwa na kuthibitishwa kuwa salama kwa afya zao na mazingira,”amesema.

Aliongeza kuwa TBS imeweka mifumo mbalimbali ya kusaidia wazalishaji kufikia viwango vinavyotakiwa, ikiwemo kutoa mafunzo, ushauri wa kitaalamu na huduma za maabara kwa ajili ya kupima bidhaa kabla ya kuingia sokoni.

Kwa mujibu wa TBS, wazalishaji ambao bidhaa zao hazijafikia viwango vinavyotakiwa hupewa ushauri wa maboresho badala ya kuzuiwa moja kwa moja, hatua inayosaidia kuongeza ubora wa bidhaa za ndani na kuimarisha ushindani wake.

Aidha,amesema TBS imeendelea kuoanisha viwango vya Tanzania na vile vya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na masoko mengine ya kikanda ili kuwezesha bidhaa zinazozalishwa nchini kuuzwa kwa urahisi nje ya mipaka ya Tanzania.

Amefafanua kuwa bidhaa zinazokidhi viwango vya ubora hupata fursa kubwa ya kupenya katika masoko ya kimataifa na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia biashara na uwekezaji.

“Tunaamini kwamba kwa kuzingatia viwango, wazalishaji wataongeza thamani ya bidhaa zao, watapata masoko mapana zaidi na kuchangia jitihada za Serikali za kukuza uchumi wa viwanda na matumizi ya nishati safi,”amesema.

Amesema kuwa TBS itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha teknolojia za nishati safi zinazozalishwa nchini zinakuwa salama, zenye ubora na zinazokubalika katika masoko ya ndani na kimataifa.