Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema takwimu rasmi zina mchango mkubwa katika kuongoza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kutoa mwongozo wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira pamoja na kupima mafanikio ya juhudi za serikali katika kujenga uchumi wa kijani na endelevu.
Afisa Masoko na Uhusiano wa NBS, Andrew Punjila,ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa Maonesho ya Wiki ya Mazingira yaliyofanyika jijini Dodoma sambamba na maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Afisa huyo amesema NBS ina jukumu la kuratibu uzalishaji wa takwimu rasmi nchini ambazo hutumika kuonesha hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kuelekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kufikia malengo ya Dira ya 2050.
Kwa mujibu wa Punjila ,Dira ya 2050 inalenga kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati wa juu.
” Takwimu ndizo zinazotuonesha tulikotoka, tulipo sasa na namna tunavyosonga mbele kufikia malengo ya kuwa na uchumi wenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja,” alisema Punjila na kuongeza kuwa
“Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kulinda mazingira kutokana na mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa na kuboresha maisha ya wananchi.”
Aidha,Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, zaidi ya asilimia 55 ya kaya nchini zinatumia kuni kwa ajili ya kupikia huku zaidi ya asilimia 56 zikitumia mkaa kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia. Kwa ujumla, zaidi ya asilimia 83 ya kaya bado zinatumia nishati ambazo si rafiki kwa mazingira na afya.
Hata hivyo, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yameongezeka kutoka asilimia 2.7 mwaka 2012 hadi zaidi ya asilimia 56 mwaka 2022 kutokana na utekelezaji wa sera, mikakati na programu mbalimbali za serikali.
Ameleza kuwa matumizi ya nishati safi yamechangia kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuboresha afya za wananchi na kuongeza muda wa kushiriki katika shughuli za uzalishaji kutokana na kupungua kwa muda unaotumika kuandaa chakula.
Punjila amesema takwimu pia zinaonesha mafanikio katika ngazi ya mikoa, ambapo Mkoa wa Dar es Salaam umefikia takribani asilimia 47 ya kaya zinazotumia nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 2.7 mwaka 2022. Alitaja pia mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Mjini Magharibi kuwa miongoni mwa maeneo yaliyoonesha ongezeko kubwa la matumizi ya nishati safi.
Punjila ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau mbalimbali vikiweno vyombo vya habari kuendelea kushirikiana na NBS katika kuhamasisha matumizi ya takwimu rasmi ili wananchi waelewe maendeleo yanayopatikana kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

More Stories
Mixx yajivunia ongezeko la Wateja kupitia kampeni yake
Airtel,Serikali waungana kupanda miti Bagamoyo na kusafisha fukwe Dar
DC Mbarali apongeza utendaji wa Mweli