November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU Kagera yaokoa zaidi ya milioni 262/-

Na Ashura Jumapili,TimejiMajira, Online Bukoba,

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kagera imeokoa sh. 262,231,702 kwa kipindi cha miezi mitatu za miradi 11 ya ushuru na miradi ya maendeleo maeneo mbalimbali ya mkoa huo yenye thamani ya sh. 3,059,004,624.08.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mkoani hapa Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, John Joseph,amesema ufuatiliaji wa miradi hiyo ulifanyika kwa miezi mitatu kuanzia Julai Mosi hadi Septemba 30 mwaka huu.

Joseph amesema katika fedha zilizookolewa, sh. milioni 117,530,600 ni mali ya halmashauri ya Biharamulo, ambapo fedha hizo zilikuwa mikononi mwa watumishi wasio kuwa waadilifu.

Kwa mujibu wa Joseph kwa nyakati tofauti katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2016/2017,2017/2018 na 2018/2019 hawakuwasilisha fedha hizo Serikalini.

“Walikuwa wakikusanya mapato kwa kutumia mashine za POS, lakini walikuwa hawawasilishi fedha hizo halmashauri na hivyo kusababisha kushindwa kutekeleza baadhi ya majukumu yake kwa ufanisi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria,”amesema.

Amesema milioni 58,760,302 zimelipwa AMCOS na SACCOS mbalimbali ambazo baadhi ya watu walikopa na kushindwa kurejesha hadi walipofuatiliwa na TAKUKURU.

Amesema AMCOS na SACCOS zilizorejeshewa fedha hizo ni pamoja na SUKARI SACCOS ya Missenyi, Biharamulo SACCOS na Benki ya Wakulima ya Mkoa wa Kagera (KFCB).

Amesema kiasi cha sh. 948,600 ni fedha zilizorejeshwa kwa wanachi wawili kutokana na mikopo umiza ambayo walikopa kwa wakopeshaji wasiokuwa na vibali vya kufanya biashara ya kukopesha.

Ameongeza kuwa sh. 18,700,600 ni fedha zilizorejeshwa kwa halmashauri ya Biharamulo kutoka kwa watumishi wawili ambao walikuwa wamejilipa kimakosa fedha za kukaimu ofisi kinyume na taratibu .