*Yaliotokea baa ya Las Vegas,baada ya watuhumiwa kumshushia kipigo mteja kisa bili sh.8,000
Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- MwanzaÂ
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limemfikisha mahakamani mshtakiwa wa tatu, Benson John (19) mlinzi (baunsa), mkazi wa Nyakabungo, Kata ya Isamilo wilayani Nyamagana mkoani hapa na kumuunganisha katika kesi ya mauaji ya Mzafuru Yunusu.
Yunusu anadaiwa kuuawa kwa kipigo katika baa ya Las Vegas iliyopo eneo la Kona ya Bwiru, mtaa wa Nyamanoro, wilayani Ilemela mkoani Mwanza,baada ya kudaiwa kushindwa kulipa bili ya sh.8000.
​Hatua hiyo imekuja Juni 3,2026, baada ya Wakili wa Serikali, Mwanahawa Changale, kuwasilisha ombi mahakamani hapo la kutaka hati mpya ya mashtaka inayomwongeza mtuhumiwa huyo ipokelewe chini ya kifungu cha 251 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
​Kufuatia marekebisho hayo ya hati ya mashtaka katika shauri la jinai namba 10492 la mwaka 2026, idadi ya washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo sasa imefikia watatu, ambao ni Yohana Peter (22) na Benson John (19) wawili hao ambao wote ni walinzi (baunsa) katika baa hiyo pamoja na Hamis Mussa (27) mfanyakazi wa usafi.
​Washtakiwa wote watatu wamepandishwa kizimbani na kusomewa shtaka hilo la mauaji mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela,Juma Opudo kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mfawidhi,Christian Mwalimu, ambaye ndiye msikilizaji wa shauri hilo.
​Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali Mwanahawa Changale, akisaidiana na Clara Muhando, aliieleza mahakama kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo Februari 5, 2026 wakiwa katika baa hiyo ya Las Vegas.
Ambapo wanadaiwa kumshambulia na kumuua Mzafuru Yunusu kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
​Hata hivyo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama ya Wilaya haina mamlaka kisheria ya kusikiliza mashauri ya mauaji, ambayo kisheria ngazi hiyo ya mahakama inayatumia kwa ajili ya kutajwa tu kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania.
​Hakimu Opudo amefafanua kuwa kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, washtakiwa hawatatakiwa kukiri au kukataa tuhuma hizo, na kuongeza kuwa kosa la mauaji halina dhamana kisheria, hivyo wataendelea kubaki mahabusu hadi pale upelelezi utakapokamilika.
​Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 17,2026 saa nne asubuhi baada ya taratibu za kisheria za kumuunganisha mtuhumiwa huyo mpya kukamilika (juzi) mahakamani.Hata hivyo washtakiwa wote watatu wamerejeshwa rumande kusubiri tarehe inayofuata ya kutajwa kwa shauri hilo.

More Stories
Wadau wahimizwa kukomesha changamoto ya Taulo za kike shuleni
Mradi wa pamba unavyosaidia kupiga vita Ajira za Watoto
Mbeya City Expo yaelimisha wananchi bidhaa bandia