OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) zimetiliana saini makubaliano ya ushirikiano kwa ajili ya utekelezaji wa Sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini na Wajenzi wa Meli Tanzania Bara, itakayofanyika katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika katika Makao Makuu ya NBS jijini Dodoma leo Juni 3,2026 Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Malick Salum, amesema kuwa tukio hilo linaashiria mwanzo rasmi wa maandalizi ya sensa ya pili ya vyombo vya usafiri majini nchini.
Amesema lengo kuu la sensa hiyo ni kukusanya takwimu sahihi na za kina kuhusu vyombo vya usafiri majini pamoja na wajenzi wa meli wanaofanya shughuli zao katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara.
“Takwimu hizo zitasaidia kubainisha idadi na aina za vyombo vinavyofanya kazi nchini, kufuatilia utekelezaji wa kanuni za usalama majini na kuweka msingi imara wa usimamizi bora wa sekta ya usafiri wa majini.” Amesema
Kwa mujibu wa Salum, sensa hiyo inafanyika kufuatia mafanikio ya sensa ya kwanza iliyotekelezwa mwaka 2021 kwa ushirikiano kati ya TASAC na NBS. Alisema sensa ya mwaka 2021 ilijikita katika vyombo vidogo vya usafiri majini vyenye urefu wa chini ya mita 24, huku sensa ijayo ikipanua wigo kwa kuhusisha vyombo vyote vya usafiri majini pamoja na wajenzi wa meli nchini.
Ameeleza kuwa matokeo ya sensa ya mwaka 2021 yalitoa picha ya awali kuhusu hali ya vyombo vya usafiri majini nchini na kuweka msingi wa kuanzishwa kwa kanzidata ya kitaifa ya vyombo vya usafiri majini.
“Sensa hiyo ilisaidia kutambua maeneo yanayotoa huduma za usafiri majini, kuwezesha ukusanyaji wa takwimu za msingi, kuboresha usimamizi wa sheria na kanuni za usalama majini pamoja na kusaidia maandalizi ya mipango kwa kuzingatia takwimu sahihi,” alisema Salum.
Aidha, amesema kabla ya sensa ya mwaka 2021, uwezo wa TASAC ulikuwa kufikia vyombo takribani 6,000 kwa mwaka kwa ajili ya ukaguzi. Hata hivyo, baada ya kupatikana kwa takwimu hizo na kuimarishwa kwa mikakati mbalimbali, shirika hilo sasa lina uwezo wa kufikia vyombo zaidi ya 21,600 kwa mwaka kwa ajili ya ukaguzi na utoaji wa vyeti.
Salum ameongeza kuwa sensa hiyo pia ilisaidia kujenga hoja ya kuongeza idadi ya wakaguzi wa vyombo vya majini, ambapo TASAC imeongeza wakaguzi kutoka 10 hadi 40 kulingana na mahitaji yaliyopo.
Amesema kutokana na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya usafiri majini, kuna umuhimu wa kufanya sensa nyingine ili kupata taarifa mpya na sahihi zaidi zitakazosaidia katika maamuzi ya kisera, udhibiti na uwekezaji. Pia alisema sensa hiyo itachangia utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya maendeleo kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Amina Msegwa, ameishukuru TASAC kwa kuendelea kuiamini NBS katika utekelezaji wa shughuli za takwimu na kuahidi ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha takwimu zitakazokusanywa zinakuwa rasmi na zenye ubora unaohitajika kwa ajili ya mipango ya maendeleo.
Msegwa amesema sensa hiyo itasaidia kutambua kwa usahihi vyombo vya usafiri majini vinavyofanya kazi katika Bahari ya Hindi, maziwa makubwa na mito mikubwa ya Tanzania.
“Tukifahamu hali halisi ya sekta hii kwa ukamilifu, tutakuwa na msingi imara wa kupanga na kutekeleza uwekezaji unaolenga kuimarisha usafirishaji wa wananchi na bidhaa nchini,” amesema.
Ameongeza kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali kubwa za maji ikiwemo bahari, maziwa na mito, hivyo sensa hiyo itasaidia kubaini namna bora ya kuunganisha usafiri wa majini na miundombinu mingine ya usafiri kama barabara na reli ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji nchini.
Msegwa amesema jitihada zinazoendelea kufanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha miundombinu na uchumi wa nchi zinahitaji kuungwa mkono na takwimu sahihi.
Amebainisha kuwa sensa hiyo itatoa majibu muhimu yatakayosaidia kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na uwekezaji zaidi kwa lengo la kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa wakati.

More Stories
Kihongosi:Viongozi msitunishiane misuli
Airtel, ZECO zaingia ushirikiano kuimarisha Huduma za Kidigitali
MSD kujenga ghala la kisasa lenye mita za mraba 3,900