June 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watu wanne wafariki kwa ajali jijini Mbeya

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WATU wanne wamefariki dunia na wengine 29 kujeruhiwa baada ya basi la abiria la Kampuni ya Mwasote lenye namba za usajili T134 DFB, aina ya Mitsubishi, kupata ajali katika barabara ya Mbeya–Chunya.

Akizungumza na waandishi wa habari June Mosi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema ajali hiyo ilitokea Mei 31, mwaka huu, majira ya saa 9:10 asubuhi katika eneo la Maji Mazuri, jijini Mbeya.

Amesema basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Nehemia Sanga (50), mkazi wa Uyole, likitokea Mbeya kuelekea wilayani Chunya, kabla ya kuacha njia na kupinduka.

Kwa mujibu wa Kamanda Kuzaga, ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu wanne, wakiwemo wanaume watatu na mwanamke mmoja. Wawili kati ya waliofariki wametambulika kuwa ni Hamza (30)na Matrida Mwabanganya mwenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya miaka 30 na 36.

Amesema watu 29 walijeruhiwa katika ajali hiyo, ambapo wanaume ni 24 na wanawake watano. Kati yao, majeruhi 11 wamelazwa hospitalini huku 18 wakipatiwa matibabu.

Majeruhi hao walikimbizwa katika Hospitali Rufaa Kanda ya Mbeya Mbeya kwa ajili ya matibabu.

Kamanda Kuzaga amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva aliyeshindwa kulimudu gari katika eneo lenye kona kali, hali iliyosababisha basi hilo kuacha njia na kupinduka.

Dereva huyo anaendelea kupatiwa matibabu akiwa chini ya ulinzi wa polisi.